Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika Mjini Babati.
………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amewapongeza wakala wa barabara za mijini na vijini (TARURA) na wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Manyara kwa namna wanavyotengeza barabara zao tofauti na mikoa mingine ya jirani.
Mkuu huyo wa Mkoa Charles Makongoro Nyerere ametoa pongezi hizo kwenye kikao cha bodi ya barabara ya Mkoa huo kilichofanyika mjini Babati.
Makongoro amesema kila anaposafiri kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara, anabaini ujenzi madhubuti umefanyika katika barabara.
“Barabara za Mkoa wa Manyara huwezi kuzifananisha na nyigine za mikoa ya jirani kwa ubora wake, nawapongeza TANROADS na TARURA,” amesema Makongoro.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema mkoa huo una mradi mmoja wa kitaifa ambao ni sehemu ya mradi wa Karatu-Mbulu-Haydom-Sibiti-Lalago-Maswa.
Mhandisi Rwesingisa amesema mradi huo wa kilomita 389 unajulikana kama Serengeti southern bypass.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 serikali imetenga sh5 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilomita 50 sehemu ya Mbulu-Haydom.
Meneja wa TARURA wa mkoa wa Manyara, mhandisi Meleck Silla amesema mkoa huo una mtandao wa urefu wa barabara za kilomita 6,759.726 zinazohudumiwa na TARURA.
Mhandisi Sillaa amesema barabara hizo zinazohudumiwa na TARURA zimegawanyika kwa barabara za lami, changarawe na udongo.
Amesema watahakikisha wanaendelea kuboresha barabara za mkoa huo ili ziweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka cha masika na kiangazi.