Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila (Katikati kulia) akisisitiza jambo wakati akizungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mikakati inayotekelezwa na mkoa huo kuongeza uzalishaji wa zao la pamba.
………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ametangaza mkakati kabambe wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba mkoani humo hatua ambayo itainua uchumi wa wakulima na kuongeza pato la taifa.
Kafulila ametangaza mkakati huo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema mkoa huo pamoja na udogo wake kwa miaka mingi umekuwa ukiongoza kwa uzalishaji pamba nchini na sasa amekuja na mikakati thabiti unaowawezesha wakulima kuona mkono wa Serikali ili kuwasaidia wafanye vizuri zaidi.
Katika utekelezaji wa mkakati huo kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa wameanzisha muundo ambao utasaidia wakulima kupata huduma bora za kilimo chini ya usimamizi thabiti na unaoeleweka.
Amesema changamoto kubwa waliyokutana nayo wakulima ni kukosekana utawala bora, kwani huko nchini (vijijini) wakulima walikuwa wakipambana wenyewe kwa wenyewe kuendesha kilimo cha pamba bila kuona mkono wa Serikali.
“Lakini mara baada ya kuanzisha muundo kuanzia ngazi ya kijiji tumeona imekuwa rahisi zaidi kwa wakulima kutekeleza maelekezo wanayoelekezwa kufanya kwa lengo la kuongeza uzalishaji,” amesema Kafulila na kuongeza;
“Muundo unaanzia ngazi wa kijiji hadi kwenye ngazi ya mkoa. Na kwenye muundo waliomo sio Serikali peke yake. Nusu ni Serikali na nusu wananchi ambao ni sehemu ya kamati ya kijiji katika kusimamia zao la pamba.”
Amesema hiyo ni tofauti na kule walikotoka ambapo ushirika kwenye ngazi ya kijiji ndiyo uliokuwa unasimamia zao la pamba. Kwa mujibu wa Kafulila madhara ya huo utaratibu ilikuwa ni upigaji kuwa mwingi na kuwajibishana kukiwa ni kidogo.
“Walipotaka kuingilia wanasema sisi ni ushirika tunajitegemea…wana siasa zao, lakini kulikuwa na kujihisi kwamba wana kinga.
Ili kuondokana na hilo, ikabidi tuanzishe muundo ambao ndani yake kuna Serikali na kukitokea jambo lolote, basi ndani yake kuna afisa wa Serikali ambaye tunaweza kumuwajibisha kwa makosa ambayo yamejitokeza pale,” amefafanua Kafulila.
Kafulila amesema kwa muundo huo kamati haihodhiwe na chama cha ushirika, lakini wanaongeza mkono wa Serikali kwenye shughuli zao. Amesema Muundo huo umeanzia kwenye kijiji, kata, ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Kwa muundo huu hata kwenye ule utaratibu wa kugawa mbegu wanahusika na kwenye manunuzi.”
Akizungumzia zao la pamba kwa ujumla mkoani humo, Kafulila alisema kwa miaka mingi asilimia 51 ya pamba yote inazalishwa kwenye mkoa huo wa Simiyu.
Amesema katika msimu uliopita kutokana na ongezeko la hamasa na kushirikisha zaidi wakuliza mkoani humo uzalishaji wa pamba uliongezeka. Alisema msimu uliopita uzalishaji wa pamba nchini kote ilikuwa kilo milioni 140, ambapo Simiyu peke yake ilizalishaji kilo milioni 81 sawa na asilimia 61 ya pamba yote iliyozalishwa nchini.
Amefafanua kuwa wao kama viongozi wanatambua kwamba pamba inasaidia sehemu kubwa ya watu wa mkoa huo wa Simiyu na inatoa mchango wake katika pato la Taifa.
Ameongeza kwamba miongoni mwa mwafanikio ya kujivunia kwa Bodi ya Pamba ni kuwa hajawahi kutokea wakulima wakapata bei nzuri ya pamba kama ilivyokuwa kwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa RC Kafulila bei ya juu kabisa ya pamba kwa mwaka huu ilikuwa sh. 1,800 wakati miaka mingine yote bei ya juu kabisa ilikuwa sh. 1,600.
Amesema bei nzuri ya pamba kwa wakulima imetokana na usimamizi na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka vitendo vya ujanja ujanja kwenye zao la pamba vinatokomezwa.
Kwa mujibu wa Kafulila moja ya changamoto ambayo ilijitokeza kwenye sekta ya pamba ni kutokana na kuwepo watu wenye nguvu waliokuwa wamekamata zao hilo na kufanya mambo wanayoyataka. Alisema tayari amekata mizizi ya watu hao na sasa biashara ya zao la pamba inafanyika kupitia utaratibu unaoeleweka.