**************
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel ametembelea na kukagua hali ya utaoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala na kuwataka kuboresha hali ya utoaji huduma kwa wateja.
Akiwa katika ziara hiyo ya kawaida, Dkt. Mollel aliwatoa hofu wafanyakazi na kuwataka kuwa kitu kimoja ilikukamilisha lengo la kusaidia Wananchi na kutoa huduma bora za tiba na kuokoa maisha ya wananchi.
“Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan amewekeza vifaa na mambo mengine na kufanya kazi nzuri sana ya kuboresha hii Hospitali hivyo nimekuja nikae na watumishi wenzangu sisi sasa tuelekee kwenye kufanya kazi haina sababu tena kwa Wananchi kulalamika.” Amsema Dkt. Mollel.
Aidha Dkt. Mollel ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kuanza kufanyia kazi changamoto zilizokuwepo awali na kuwataka kujikita zaidi katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi na nidhamu kazini.
“Mimi niwapongeze, nimeingia kwenye idara ya akina Mama pale nimeona kwamba akina mama wanasema wanasikilizwa na wanahudumiwa kwa wakati tena manesi wanawanyenyekea” ameeleza Dkt. Mollel.
Katika kuhakikisha wafanyakazi hao wanaendelea kufanya vyema hasa wale wa wodi ya wazazi, Dkt. Mollel aliweza kuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuwapa motisha watumishi watatu kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wateja wao.
Dkt. Mollel amesema kuwa ndani ya miezi mitano hali halisi ndani ya Hospitali hiyo imebadilika huku akisema kuwa matukio ya malalamiko anasubiria tume waliyoiunda kuja na taarifa na mapendekezo ya kuboresha zaidi hali ya utoaji huduma za afya.
Ameeleza kuwa mfumo wa kushughulikia matatizo yameelekezwa kwa kuanzia viongozi wa juu hadi chini hivyo kila mkuu wa idara ashughulikie changamoto katika idara yake kwa ukamilifu.
Kwa upande wake Mganga mkuu Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Zavery Benela alisema kuwa Hospitali hiyo licha ya kuwa na changamoto karibu huduma nyingi zimeboreshwa na wanafanya vizuri.
“Kwa sasa hospitali tunatoa na kuendelea kutoa huduma za kibingwa ikiwemo idara ya upasuaji, pua na koo, magonjwa ya ndani, magonjwa ya ngozi, kinywa na meno kwa watoto na kwa siku tunahudumia wastani wa wagonjwa 1600 hadi 2000” Amesema Dkt. Benela
Mwisho