……………………………………………
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO, Mbeya
Mpango wa pili wa kuhamasisha njia za kujikinga na UVIKO-19 ikiwemo kupata chanjo ya CORONA unaendelea nchi nzima, ambapo Serikali imedhamiria kumfikia kila Mtanzania kwa kuwafuata katika maeneo yao ya makazi, biashara, starehe na kazi.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Igawa, Dkt. Sudi Magoto ameeleza kuwa, awamu hii ya pili wameweza kuwafikia watu wengi zaidi ambao wanashindwa kufika katika Vituo vya Afya kutokana na umbali.
Dkt. Sudi alisema hayo, jana Desemba 27, 2021 wakati timu ya Taifa ya mpango wa pili wa kuhamasisha njia za kujikinga na UVIKO-19 ikiwemo kupata chanjo ya CORONA ilipofika Zahanati hapo kuona namna zoezi la utoaji chanjo linavyoendelea katika kata ya Igawa, wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
“Tunapoenda vijijini kutoa elimu na chanjo ya CORONA, tumekuwa tukiwatumia Wenyeviti wa Mitaa ambao wanatoa matangazo kwa jamii, baada ya Wananchi kukusanyika tunawaelimisha kuhusu ugonjwa wa CORONA, namna ya kujilinda na baadae tunatoa chanjo,” alisema Dkt. Sudi.
Aliendelea kusema kuwa, mpango huu wa pili umeweza kuwafikia watu wengi zaidi, kutokana na maeneo mengi ya vijijini kuwa mbali hivyo watu kushindwa kufuata huduma ya chanjo kwenye Zahanati kutokana na umbali.
Ameendelea kusema kuwa, kwa siku wamekuwa wakichanja zaidi ya watu kumi (10) wengi wao wakiwa ni Wanawake.
Kwa upande wake, Muuuguzi wa Afya, Hospitali ya Wilaya ya Mbarali, Evarada Mapunda, amesema muitikio wa kuchoma chanjo ni mkubwa, watu wengi wanajitokeza kwenda kuchoma chanjo hospitalini hapo.
“Wagonjwa wanapokuja kwa ajili ya matibabu, huwa tunawapa elimu ya ugonjwa wa CORONA na faida ya kuchanja ambayo ni kupunguza makali ya ugonjwa huo na muitikio umekuwa ni mkubwa,” alisema Evarada.
Aliendelea kusema kuwa, tangu awamu ya pili ya utoaji chanjo ya CORONA uanze tarehe 22 hadi 26 Desemba, 2021 wamechanja watu 70.
Mpango wa pili wa kuhamasisha njia za kujikinga na UVIKO-19 ikiwemo kupata chanjo ya CORONA ulizinduliwa Jijini Arusha na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, Desemba 22, 2021 na baadae zoezi hilo liliendelea nchi nzima.