*********************
NA VICTOR MAKINDA: MOROGORO
Wakati tunaelekea kuumaliza mwaka 2021 na kuanza mwaka 2022, Wito umetolewa kwa Wanawake wajane kujiwekea malengo na mikakati mathubuti ya kufanya shughuli za uzalishaji mali ili waweze kumudu gharama za maisha na malezi ya watoto.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa asasi isiyo ya Kiserikali ya UECO, Sophia Kalinga,ambaye pia ni mjane, wakati wa kongamano la wanawake wajane wa Manispaa ya Morogoro lililofanyika jana mjini hapa .
Akizungumza katika kongamano hilo, Kalinga amesema kuwa ujane sio laana hivyo wanawake wajane wasijione kuwa hawawezi kusimama peke yao, bali wanatakiwa kujithatiti katika kufanya shughuli mbali mbali za uzalishaji mali ili waweze kumudu kulea familia walizoachiwa na waume zao.
“Achane kuhuzunika, tumieni fursa za mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha, undeni vikundi vya ujasiriamali, Halmashauri zetu zina fungu maalumu la mikopo ya ujasiriamali kwa ajili ya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu, msiogope, mwende mkakope, jambo la msingi ni kujiwekea malengo na kujidhatiti kikamilifu katika kufanya kazi kwa bidii.” Alisema Sophia.
Sophia aliwataka wanawake wajane na wale ambao wanalea watoto pasipo baba ‘Single Mothers’ kujiepusha na mahusiano ya mapenzi holela kwani kufanya hivyo hakutawapa unafuu wa maisha bali wanaweza kuambukizwa magonjwa ya ngono ikiwa ni pamoja na UKIMWI, yatakayopelekea kuwaacha watoto wao yatima.