………………………………………………….
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MASELE LIGE [30] Mchimbaji wa Madini ya Dhahabu na Mkazi wa Kijiji cha Ujerumani kwa tuhuma za mauaji ya MHOJA MADALE MIHAMBO [30] Mchimbaji wa Dhahabu na Mkazi wa Ujerumani – Chunya.
Tukio hili limetokea mnamo tarehe 24.12.2021 majira ya saa 06:30 alfajiri huko Kitongoji cha Ujerumani, Kata ya Mkola, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya na Mkoa wa Mbeya ambapo mtuhumiwa akishirikiana na mwenzake aliyefahamika kwa jina moja la CLEMENT ambaye alikimbia baada ya tukio hili walimuuaa MHOJA MADALE MIHAMBO kwa kumpiga na sululu kichwani maeneo ya kisogoni.
Chanzo cha tukio ni kugombania chakula kwa madai kwamba marehemu alikua hatoi michango ya chakula mara wauzapo Dhahabu. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kutenda kosa hilo kwa kushirikiana na mwenzake. Msako mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa aliyekimbia. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.
ASAKWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamsaka mtu aliyefahamika kwa jina moja la LOLE, Mkazi wa Kiwanja Wilaya ya Chunya kwa tuhuma za mauaji ya SAMWEL CHISUNGA [19] Mkazi wa Mbozi – Mkoa wa Songwe kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa fimbo.
Tukio hili limetokea mnamo tarehe 25.12.2021 majira ya saa 05:00 alfajiri huko Kijiji cha Mlimanjiwa, Kata ya Mbugani, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Chanzo cha tukio ni marehemu kuiba Omega/unga udhaniwayo kuwa na dhahabu mali ya mtuhumiwa. Msako wa kumtafuta mtuhumiwa ambaye alitoroka baada ya kutenda tukio hili unaendelea.
ASAKWA KWA TUHUMA ZA KUJERUHI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamsaka SOMBWILE ANGANILE MWAKASAMBWE Mkazi wa Ikolo – Wilaya ya Kyela kwa tuhuma za kumjeruhi PAULINA LUKANI MWAIKUPA [41] Mkazi wa Ikolo kwa kushambuliwa na kitu chenye ncha kali na kumsababishia jeraha eneo la ubavu wake wa kulia.
Tukio hili limetokea mnamo tarehe 25.12.2021 majira ya saa 23:00 usiku huko Kijiji na Kata ya Ikolo, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Chanzo cha tukio ni tamaa za kingono, inaelezwa kuwa wakati wa tukio mhanga alikuwa amelala ndani ya nyumba yake ghafla mtuhumiwa aliingia kwa nia ya kufanya shambulio la aibu lakini mhanga alipomwona alipiga kelele za kuomba msaada ndipo mtuhumiwa kwa hasira alitoa kisu na kumjeruhi. Mhanga amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kyela kwa matibabu. Msako mkali unaendelea wa kumtafuta mtuhumiwa.
KUPATIKANA NA POMBE YA MOSHI [GONGO].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia REHEMA MAKANYIKA [35] mkazi wa Sae Jijini Mbeya akiwa na Pombe ya Moshi [Gongo] lita 05.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 24.12.2021 majira ya saa 11:40 asubuhi katika msako uliofanyika huko Sae, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia CHRISPIN MTAMBO [28] mkazi wa Airport ya Zamani Jijini Mbeya na wenzake 03 wakiwa na bhangi yenye uzito wa Gram 22.5.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 24.12.2021 majira ya saa 11:00 asubuhi huko Sae, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya katika Misako inayoendelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MSUMBUKO PATSON [31] Mkazi wa Kijiji cha Matundasi aliyekuwa anatafutwa kwa kosa la mauaji alilotenda tarehe 14.08.2019 huko Wilayani Chunya.
Mtuhumiwa amekamatwa mnamo tarehe 25.12.2021 majira ya saa 20:00 usiku katika msako uliofanyika huko Kijiji na Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Ni kwamba mnamo tarehe 14.08.2019 mtuhumiwa alimuua mtu aliyefahamika kwa jina moja la NDUGUSU na kisha kukimbia. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kosa hilo. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia 1. SUBIRA MWANDAMBO [34] Mkazi wa Mlimanjiwa na 2. SAIMON MWAMBENDE [40] Mkazi wa Mlimanjiwa wakiwa Pombe Moshi (Gongo) lita 20.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 25.12.2021 majira ya saa 23:30 usiku huko Kijiji cha Mlimanjiwa, Kata Mbugani, Tarafa Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye klabu chao cha Pombe za Kienyeji wakiuza Pombe hizo kwa kuchanganya na Pombe Haramu ya Gongo.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye MWINGA ZAKAYO [17] Mkazi wa Kikuyuni akiwa na kete 07 za Bhangi ndani ya chumba chake zikiwa kwenye mfuko wa kaki.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 25.12.2021 majira ya saa 09:15 asubuhi huko Stendi mpya ya Makongolosi iliyopo Kitongoji cha Mkaongolosi, Kata ya Mkaongolosi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji wa dawa hizo za kulevya.
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.