Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza (kulia) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kushoto) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Jaffary Mpina (wa pili – kushoto). Viongozi hao walikuwa katika ziara ya kazi Desemba 23, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Malassa (katikati), akizungumza na viongozi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy (wa kwanza-kushoto), walipokuwa katika ziara ya kazi Desemba 23, 2021.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kulia) wakijadiliana jambo wakati walipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Kibondo kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Desemba 23, 2021.
Kazi ya kufunga miundombinu ya umeme ikiendelea katika kijiji cha Kagezi, wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma wakati Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (hawapo pichani) walipokuwa katika ziara ya kazi, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Desemba 23, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Malassa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili – kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa pili – kulia) na Wataalamu kutoka REA na TANESCO. Ujumbe huo ulikuwa katika ziara ya kazi Desemba 23, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza (wa pili – kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa tatu – kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa kwanza-kulia) na Wataalamu kutoka REA na TANESCO. Ujumbe huo ulikuwa katika ziara ya kazi Desemba 23, 2021.
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Malassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy wakijadiliana jambo. Viongozi wa REA walimtembelea Mkuu wa Wilaya wakiwa katika ziara ya kazi, Desemba 23, 2021.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, wakikagua kazi ya uchimbaji mashimo kwa ajili ya kusimika nguzo za umeme, inayoendelea katika kijiji cha Kagezi wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma. Viongozi hao walikuwa katika ziara ya kazi, Desemba 23, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Evance Malassa (kushoto) akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kulia) baada ya kikao baina ya Ujumbe kutoka REA ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (hayupo pichani) na Mkuu wa Wilaya, Desemba 23, 2021.
*******************************
Na Veronica Simba – Kigoma
Imeelezwa kuwa Mpango Kabambe wa Kupeleka Nishati Vijijini umelenga kuwanufaisha wananchi kupitia usambazaji umeme pamoja na nishati bora ya kupikia.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Kigoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy, walisema kuwa Mpango huo unahusisha nishati za aina mbalimbali, siyo umeme peke yake.
Wakili Kalolo alisema kuwa, ni jukumu la REA kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziwasaidie kuboresha maisha yao, hivyo Wakala umejiwekea mikakati ya kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa ipasavyo.
Akifafanua, alisema kuwa REA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na inaendelea kufanya vema katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hivyo hakuna shaka katika utekelezaji wa miradi ya aina nyingine za nishati zilizofanyiwa tafiti, utakuwa wenye ufanisi pia.
Akitoa mfano, alisema kuwa tafiti zinaonesha eneo jingine muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ni katika nishati ya kupikia ambapo asilimia kubwa ya waathirika ni wanawake, ambao kutokana na matumizi ya kuni, wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya macho na kifua.
Alisema, ni kwa sababu hiyo, Wakala umedhamiria kuondoa adha hiyo katika jamii hususani wanawake waishio vijijini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu akidadavua zaidi kuhusu Mpango huo kabambe, alieleza kuwa umejikita katika sehemu mbili kubwa ambazo ni usambazaji umeme pamoja na nishati ya kupikia.
Alieleza zaidi kuwa, hivi sasa, Wakala unaongeza nguvu zaidi katika nishati ya kupikia ili kuhakikisha kwamba wananchi hususan wa vijijini, wanatumia nishati bora kwa shughuli za kupikia na kupunguza au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa ambao upatikanaji wake ni mgumu, aghali na siyo rafiki kwa mazingira.
Mhandisi Saidy alisema REA imefanya tafiti kadhaa za majaribio kuhusu nishati ya kupikia mathalani mradi wa kutumia tungamotaka, ambapo mifumo husika ilipelekwa katika maeneo 725 yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.
Aidha, aliongeza kuwa, Wakala umeshirikiana na kampuni za usambazaji gesi kufanya tafiti kuhusu uwezekano wa kuhakikisha nishati ya gesi inafikishwa katika maeneo ya vijijini kwa gharama nafuu ili wananchi waweze kuitumia kwa shughuli za kupikia.
Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwahakikishia Wakuu wa Wilaya za Kibondo na Kakonko, ambao walikutana nao kwa nyakati tofauti, kuwa maeneo yote ya kimkakati, hasa yanayohusisha masuala ya usalama yatapelekewa huduma ya umeme ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa ufanisi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Malassa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Kanali Aggrey Magwaza, kwa nyakati tofauti waliomba maeneo ya mpakani ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme, yapewe kipaumbele katika kufikishiwa nishati hiyo ili kuimarisha shughuli za kiusalama.
Pia, Wakuu hao wa Wilaya walipongeza jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Wakala wa Nishati Vijijini katika kusambaza umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu pia walikagua miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kukutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ambapo walijadili changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Kupitia kikao hicho, viongozi hao waliipatia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji vifaa iliyokuwa ikimkabili Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Kampuni Tanzu ya TANESCO (ETDCO) katika wilaya za Kakonko na Kibondo.
“Utekelezaji ulikuwa nyuma kidogo kutokana na changamoto ya vifaa. Tumetatua changamoto hiyo na tumemwelekeza Mkandarasi ndani ya miezi mitatu awe amekamilisha mradi huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu.
Aidha, Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo katika wilaya za Buhigwe, Kasulu, Kigoma Vijijini na Uvinza, Kampuni ya M/s CCCE Etern Consortium alielekezwa kuongeza nguvu ili akamilishe kazi hiyo kwa wakati uliopangwa ambao ni mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba, 2021.
Miradi mingine inayotekelezwa mkoani Kigoma ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kuanza hivi karibuni pamoja na Mradi wa Ujazilizi unaolenga kufikisha umeme katika maeneo yaliyopitiwa na miundombinu ya nishati hiyo lakini umeme haujashushwa.
Katika ziara hiyo, viongozi hao wa REA waliambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Wakala hiyo pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)