Rozaria Daniel kushoto anayeishi katika kituo cha kulea watoto yatima cha St Antony Mfaranyaki katika Manispaa ya Songea kushoto akipokea zawadi kutoka kwa Msamaria mwema Edwina Daniel ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro jana ambapo familia ya Dkt Ndumbaro ilitembelea na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika vituo mbalimbali vya kulea watoto wenye mahitaji maalum,Mbunge wa Jimbo la Songea mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro kushoto akifurahi jambo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano kulia baada ya kukabidhi misaada mbalimbali kwa watoto yatima wanaoishi katika kituo cha Swako kata ya Mwengemshindo,katikati ni Diwani wa kata hiyo Osmund Kapinga.
Mbunge wa Jimbo la Songea mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro wa pili kushoto akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa Mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaotoka kwenye mazingira magumu cha Swako kilichopo kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea Regina Chingulu wa pili kulia baada ya Waziri kutembelea kituo hicho jana ambapo alitoa msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto hao huku Mamlaka ya Uhifadhi wanyamapori ikitoa vitanda na magoro,wa kwanza kushoto Kamanda wa Uhifadhi Wanyamapori Kanda ya Kusini Abraham Jullu na kulia Meneja wa kituo cha Swako Castory Whero.
Mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya St Exavery iliyopo Mkongo wilayani Namtumbo Emakulatha Mgomea kushoto akipokea zawadi kutoka kwa mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Songea mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro Daniel Ndumbaro wakati familia ya Dkt Ndumbaro ilipotembelea kituo cha kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha St Antony Mfaranyaki mjini Songea.
Picha na Muhidin Amri
****************************
Na Muhidin Amri,
Songea
MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damas Ndumbaro,ametembelea na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum wanaoishi katika vituo vitatu vya St Antony Mfaranyaki,Swako cha Mwenge Mshindo na St Teresa kilichopo kata ya Msamala.
Zawadi zilizotolewa kwa watoto hao ni mchele,sabuni za unga,mafuta ya kupaka,Daftari,kalamu,peni,mafuta ya kula uku Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori(Tawa)imetoa vitanda na magodoro kwa kituo cha Swako.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vitu hivyo Dkt Ndumbaro alisema, lengo la kutoa zawadi hizo ni kushiriki pamoja na watoto hao wakati huu wa sikukuu ya Chrismas na Mwaka mpya hasa ikizingatia kuwa bado watoto hao ni wadogo wanaohitaji msaada.
Alisema, amefanya hivyo kutokana na kutambua umuhimu wa mahitaji kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao baadhi yao hawana wazazi na walezi wanaoweza kuwasaidia mahitaji ya kila siku.
Dkt Ndumbaro,ameitaka jamii na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia watu wenye mahitaji na makundi maalum ili nao waishi maisha ya furaha kama ilivyo kwa watu wengine.
Aidha,amelishukuru Jimbo kuu la Songea kwa kuanzisha kituo cha kulea watoto wenye mahitaji maalum ambacho kimesaidia sana kutunza watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema, Jimbo la Songea mjini ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine hapa nchini kwani limedhihirisha na kuonesha upendo mkubwa kwa kuanzisha vituo vya kulea watoto katika maeneo mbalimbali,hatua iliyosaidia baadhi ya watoto yatima kupata mahali pa kuishi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano alisema,jambo hilo ni faraja kubwa sio kwa watoto tu bali hata kwa watu walioamua kuwakusanya na kuwatunza watoto hao katika vituo maalum.
Naye mlezi wa kituo cha St Antony Mfaranyaki Sister Judith Mwageni alisema, katika kituo hicho kuna watoto 64 kati yao wapo wanaosoma shule ya Msingi na Sekondari ambao wanahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake Baraka Mvulla, ameishukuru familia ya Dkt Ndumbaro kwa kuonesha upendo mkubwa kwao kwani haijawahi kutokea kituo hicho kupelekea msaada mkubwa kama ilivyofanya familia ya Waziri Ndumbaro.
Mvulla,amewaomba watu na jamii kuendelea kuwasaidia kwani licha ya kutunzwa katika kituo cha kanisa,hata hivyo wanahitaji vitu mbalimbali kwa ajili ya masomo na maisha yao ya kila siku.
Naye Meneja wa kituo cha Swako kilichopo kata ya Mwengemshindo Abraham Jullu amemshukuru Dkt Ndumbaro kwa msaada huo na kueleza kuwa,huo ni upendo unaopaswa kuigwa na wadau wengine.
MWISHO.