……………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Wakazi wa Kijiji Cha Lorbene Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamesikitishwa na kitendo cha shule ya msingi Lorbene alipozaliwa mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka kuwa ya mwisho kwa ufaulu.
Kiwilaya shule hiyo ya msingi Lorbene imeshika nafasi ya 41 kati ya shule 41, kimkoa ya 215 kati ya shule 216 ambapo wanafunzi 10 walifanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu.
Wakizungumza kwa masikitiko wakazi hao wamedai kuwa kitendo cha kushika nafasi ya mwisho kwa shule ya msingi ya kijiji cha Lorbene nyumbani alipozaliwa mbunge Ole Sendeka kimewasikitisha mno.
Mmoja kati ya wakazi hao Saitoti Kimeso amesema mbunge huyo alipaswa kuipa kipaumbele shule hiyo ili ifanye viziri kwenye taaluma na siyo kushika nafasi ya mwisho.
Saitoti amesema mbunge anasomesha watoto wake nchini Kenya ndiyo sababu hajali kuboresha taaluma ya shule hiyo wanaosoma watoto wa wanakijiji wenzake.
Amesema Ole Sendeka amezaliwa kwenye kitongoji cha Losokonoi Kijiji cha Lorbene hivyo anapaswa kuijali shule ya kijiji alichozaliwa.
“Anapaswa kupambania maboresho ya elimu na siyo kuongoza harakati za kumfukuza ofisa elimu ya msingi wa wilaya Silvanus Tairo ambaye anajitahidi kunyanyua elimu ya wafugaji,” amesema.
Amesema ni bora mbunge huyo ashirikiane na idara ya elimu kuboresha taaluma kuliko kuwa na vinyongo na kuwatupia mzigo kuwa walimu ndiyo walisababisha akakosa ubunge mwaka 2015.
Mkazi mwingine John Mollel amesema mbunge huyo anapaswa kuiga nyayo za mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea Saniniu Laizer ambaye amejenga shule ya mtaala wa kiingereza kijiji kwao.
“Nyumbani ni nyumbani hivyo tunapaswa kupaboresha kwanza kuliko sehemu nyingine kwani ndiyo mahali tumezaliwa na kuanza maisha yetu hapa duniani,” amesema Mollel.
Hata hivyo, mbunge huyo amesema shule zote za wilaya ya Simanjiro ni zake hivyo hakuna shida shule ya Lorbene kuwa ya mwisho.
Ole Sendeka amesema yeye siyo Mwenyekiti wa kitongoji au kijiji hivyo hausiki na shule za vijiji kwanj shule zote za wilaya ni zake.
“Kwani kwenye wilaya ya Simanjiro haitakiwi kuwepo na shule ya kwanza na shule ya mwisho? hiyo shule hata ikiwa ya mwisho kuna tatizo gani?” amehoji Ole Sendeka.