Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro kulia akimkabidhi vifaa vya kupima unyevu na ubora wa zao la korosho katikbu wa Chama cha msingi cha ushirika Sama Amcos Rashid Mbutuka vilivyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd).
Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani kushoto na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro kulia wakiangalia vifaa vya kupima unyevu na ubora wa korosho vilivyotolewa kwa vyama vya msingi vya ushirika wilayani humo kwa ajili ya kudhibiti ubora wa zao.
……………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
CHAMA kikuu cha Ushirika wilaya Tunduru mkoani Ruvuma(Tamcu Ltd), kimesambaza vifaa vya kupima unyevu na ubora wa korosho vyenye thamani ya Sh.milioni 218,230,000.00 kwa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) vinavyokukusanya na kuuza korosho za wakulima.
Meneja Mkuu wa Tamcu Imani Kalembo alisema, usambazaji wa vifaa hivyo umetokana na maamuzi ya mkutano mkuu wa wadau wa zao la korosho mwaka 2019 ulioagiza katika msimu wa 2019/2020 kila chama cha msingi(Amcos)kinunue vifaa vya kupima unyevu wa korosho na mizani ndogo.
Alisema,kufuatia uamuzi huo Bodi ya Tamcu Ltd ilitangaza zabuni na kampuni ya Dirma Holding ndiyo iliyoshinda na kupewa kazi ya kusambaza vifaa hivyo.
Alisema, kwa kuwa bei ya vifaa hivyo ni kubwa,Bodi ya Tamcu imeamua kuagiza kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza zimeagizwa mizani 100 na kila moja imenunuliwa kwa Sh.1,422,300.00 na vipima unyevu(Moisture Meters)100 ambazo zimenunuliwa kwa Sh.760,000.00 kwa kila moja.
Alisema,vifaa hivyo vimeagizwa kwa mkopo ambapo Tamcu Ltd ndiyo wadhamini wa mikopo hiyo kwa niaba ya vyama vya Ushirika vya msingi na Amcos zitalazimika kulipa ndani ya misimu miwili ya mauzo ya korosho 2021/2022 na 2023.
Kalembo alisema, ugawaji huo wa vifaa umezingatia uzalishaji wa korosho kwa kila chama cha ushirika cha msingi na una lengo la kuongeza uzalishaji na kuimarisha ubora wa zao hilo linaloingiza fedha nyingi katika wilaya hiyo kongwe hapa nchini.
Meneja wa Bodi ya Korosho Tawi la Tunduru Shauri Mokiwa, ameipongeza Bodi ya Tamcu kwa kuona umuhimu wa kununua vifaa hivyo kwani vitasaidia sana wakulima kuuza korosho bora kwenye minada na hivyo kujipatia fedha nyingi.
Alisema,korosho zinazalishwa wilayani Tunduru lakini walaji(wateja)wako nje ya nchi,kwa hiyo bila kuchukua hatua za kudhibiti ubora kuna hatari ya kuharibika wakati wa utunzaji na zinaposafirishwa kwenda kwa wateja.
Amewataka viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika,kuhakikisha wanakwenda kutumia vifaa hivyo kuongeza ubora wa zao la korosho zinazofikishwa kwenye maghala ili kuwasaidia wanachama ambao ni wakulima.
Akizungumza na viongozi wa vyama vya msingi na Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema, vifaa hivyo vinakwenda kuimarisha na kulinda zao la korosho ambalo limekuwa chachu kubwa ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Amewakumbusha wadau wa zao korosho wilayani humo,kuhakikisha wanalinda kwa zao hilo kwa nguvu zote ili liendelee kuleta tija kwa wakulima na serikali ipate mapato ambayo yatasaidia kuboresha huduma za kijamii.
Amevitaka vyama vya msingi vya ushirika vilivyopata mkopo huo,kulipa madeni kwa wakati,kulinda na kutunza vifaa hivyo ili vitumike kuimarisha zao la korosho badala ya kwenda kutumia kinyume na malengo husika.
Alisema vifaa hivyo vimenunuliwa na Tamcu, hata hivyo Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa viongozi wa Amcos watakaye bainika kutumia vibaya au kupoteza vifaa hivyo.