Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu kulia,akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nampungu kata ya Nampungu wilayani Tunduru ambapo amewataka kufanya kazi za kujiletea maendeleo na kushiriki kazi za kujitolea pamoja na kujiandaa kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika mwezi Agosti mwakani,kushoto ni makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Said Bwanali.
*****************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WAKAZI wa vijiji vya Mbatamila,Kitalo na Nampungu kata ya Nampungu wilayani Tunduru,wanalazimika kutembea umbali wa km 28 kwa miguu kwenda katika maeneo mengine kufuata mahitaji na huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya.
Hali hiyo inatokana na ubovu wa barabara ambayo imeharibika vibaya kuanzia kata jirani ya Nandembo hadi Nampungu, ambapo magari ya abiria yamesitisha safari zake hali inayowalazimu wananchi wa vijiji hivyo kutumia usafiri wa malori na pikipiki ambao sio salama sana.
Wakitoa kilio chao kwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu walisema, barabara hiyo kwa sasa imeharibika sana kwa kuwa na mashimo makubwa na mifereji midogo ya maji inayopita katikati ya barabara kutokana na mvua zilizonyesha miaka miwili iliyopita na iliachwa bila kufanyiwa matengenezo.
Rashid Mwakambaya ameiomba Serikali kupitia wakala wa barabara mjini na vijijini (Tarura),kufanya matengenezo ya haraka barabara hiyo kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha ili waweze kuitumia katika shughuli za maendeleo ikiwemo kusafirisha mazao kwenda sokoni.
Mwajuma Ali alisema, wananchi husasani wanawake wajawazito wa vijiji vinavyunda kata ya Nampungu wanashindwa kwenda Hospitali ya wilaya kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao na watoto waliopo tumboni kutokana kukosekana kwa usafiri wa uhakika jambo linalo hatarisha maisha yao.
Diwani wa kata hiyo Jaffar Fundi alisema kama serikali itachelewa kuchukua hatua za haraka basi kuna uwezekano mkubwa wa kukatika kwa mawasiliano kati ya vijiji vya kata ya Nampungu na maeneo mengine.
Hata hivyo,amewataka wananchi wa kata hiyo kuwa na utaratibu wa kujitolea nguvu zao na kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya jukumu hilo kuiachia serikali.
Alisema,licha ya kijiji cha Nampungu kuanzishwa kwa muda mrefu,lakini bado kipo nyuma kimaendeleo kutokana na wakazi wake kusua sua katika suala la kujitolea nguvu na fedha, hivyo kusababisha kuchelewa kwa maendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu alisema,serikali imeshatoa Sh.milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika na wananchi waitumie kusafiri na kusafirisha mazao hasa za maarufu la korosho kwenda katika minada.
“ndugu zangu napenda kuwajulisha kwamba fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii zipo na mkandarasi ameshapatikana ambaye amehaidi kufanya kazi hata wakati wa masika ili kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa”alisema Kungu.
Kungu, amewaomba wananchi hao kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan ambaye tangu alipoingia madarakani amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha amewahakikishia kuwa,yeye kama Mbunge atashirikiana na serikali kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo na Jimbo la Tunduru Kaskazini ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya kazi za maendeleo,ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kujitolea na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Alisema,barabara hiyo imechelewa kujengwa kwa sababu mkandarasi aliyepewa kazi hiyo alikuwa anajenga barabara nyingine ya Nakapanya-Tuilieni na barabara ya Namakambale kwenda Tinginya na ile inayoelekea Ngapa ambapo tayari amemaliza na wiki ijayo ataanza kujenga barabara ya Nandembo-Nampungu.
Naye Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Mhandisi Silvanus Ngonyani alisema,mkandarasi kampuni ya MS Mucha Bulding Ltd alitakiwa kuanza kazi tangu tarehe 6 Desemba,lakini hadi sasa bado hajafika eneo la mradi kutokana na changamoto ya kifedha.
Alisema,muda wa ujenzi wa barabara hiyo ni miezi mitano ambapo kwa mujibu wa mkataba mkandarasi anatakiwa kukamilisha kazi hiyo Mwezi April mwakani.
MWISHO.