Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manayara, Mhandisi Walter Kirita akisoma taarifa ya RUWASA mjini Babati kwenye kikao cha wadau wa maji wa Mkoa huo.
…………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Babati
MKOA wa Manyara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 umeidhinishiwa kutumia shilingi bilioni 16.176 ili kujenga miradi mipya 34 na kukarabati skimu za zamani 10.
Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, mhandisi Walter Kirita, ameyasema hayo Mjini Babati wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za RUWASA kuanzia Julai hadi Novemba mwaka huu kwenye kikao cha wadau wa maji.
Mhandisi Kirita amesema fedha hizo zitaongeza mtandao wa miradi 13 na kuchimba visima 39.
“Miradi hii itasogeza huduma ya maji kwenye vijiji vipya 57 kwahiyo ifikapo Juni 2022 idadi ya vijiji ambavyo havina huduma ya uhakika itapungua kutoka vijiji 148 hadi vijiji 91,” amesema mhandisi Kirita.
Amesema fedha ambazo zimepokelewa kwenye kila Halmashauri ni Hanang’ shilingi bilioni 3.45, Mbulu Mji shilingi milioni 318.1, Kiteto shilingi bilioni 2.4.
Amesema Halmashauri ya wilaya ya Mbulu shilingi bilioni 2.8, Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro shilingi bilioni 3.5, Babati Mji shilingi milioni 732 na Halmashauri ya Wilaya ya Babati shilingi bilioni 2.2.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Wakili msomi Dokta, Suleiman Serera amesema moja ya taasisi zinazompa usingizi mzuri kwenye eneo hilo ni RUWASA kutokana na uchapakazi wao.
“Tatizo lililopo ni kutoidhinishwa kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Simanjiro Johanes Martin kushika nafasi hiyo kwani bado ana kaimu nafasi hiyo tuu hajaidhinishwa,” amesema Dokta Serera.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Caroline Mthapula amewataka RUWASA kwenda kupanga vizuri mpango wao ili vijiji vyote viweze kupata huduma.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Rose Kamili amesema RUWASA wanafanya kazi nzuri.
Kamili amewashauri RUWASA kuwa na bei moja ya maji siyo wengine wanauziwa ndoo moja ya lita 20 shilingi 50 na wengine shilingi 20.