Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora kamishna msaidizi ACP Richard Abwao akiwa na mtemi wa sungusungu Kalenjini Malembeka pamoja na mkuu wa polisi wilaya ya Igunga Ally Mkalipa wakifanya mazoezi na jeshi la jadi sungusungu baada ya kuwasili katika kijiji cha Bukama kata ya Mbutu wilayani Igunga mkoani Tabora
Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora kamishna msaidizi ACP Richard Abwao wa pili kutoka kushoto na aliye katikati mkuu wa polis wilaya ya Igunga Ally Mkalipa na wanne mtemi wa Sungusungu wilaya ya Igunga Kalenjini Malembeka wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi walio nyuma yao baada ya kumaliza mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bukama kata ya Mbutu wilayani Igunga mkoani Tabora.
………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Tabora kamishna msaidizi ACP Richard Abwao amewatumia salamu watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ikiwemo vya ujambazi wa kutumia silaha na kusema kuwa hakuna atakayebaki salama kwa kuwa mkoa wa Tabora sio sehemu ya kufanyia majaribio kwani polisi na sungusungu wanafanya kazi za doria usiku na mchana katika maeneo yote.
Ambapo aliwaagiza wakuu wa vituo vya polisi wilaya kata katika mkoa wa Tabora kushirikiana kwa pamoja na majeshi ya jadi sungusungu kuwasaka wahalifu na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.
Alitoa maagizo hayo kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Bukama kata ya Mbutu wilayani Igunga mkoani Tabora alipokuwa akizungumza na wananchi pamoja na jeshi la jadi sungusungu katika ziara yake ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya polisi na jeshi la jadi kuwa na ushirikiano wa pamoja wa kukabiliana na vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.
Kamanda Abwao alisema ili kukomesha vitendo vya uhalifu mkoa wa Tabora lazima wananchi washirikiane na jeshi la polisi ikiwemo kuunda jeshi la sungusungu kupitia viongozi wao wa vitongoji, vijiji, kata na tarafa wilaya hadi ngazi ya mkoa.
Alisema wahalifu wengi wamekuwa wakijificha katika jamii huku wakifanya uhalifu na baadhi ya wananchi wakiwaficha pasipo kutoa taarifa katika vyombo vya dora.
Aliisema kufuatia hali hiyo ndiyo maana jeshi la polisi limekuwa likikwama kuwakamata baadhi ya wahalifu ambao wamekuwa wakijificha katika maeneo yao ya jamii isiyo na matendo yasiyo ya uhalifu.
Hata hivyo kamanda Abwao alisema changamoto nyingine kubwa inayowakabili jeshi la polisi ni upungufu wa askari kwani askari mmoja anapaswa kwa wastani kulinda wananchi 400 lakini hivi sasa askali mmoja analinda wananchi 3709 hali hiyo ni changamoto kubwa.
Alisema endapo wananchi wataunda jeshi la jadi sungusungu kila eneo wakashirikiana na jeshi la polisi kuwadhibiti wahalifu kila kona vitendo vya uhalifu vitapungua au kuisha kabisa katika mkoa wa Tabora.
Aidha Abwao kupitia mkutano huo alitoa wito kwa jeshi la sungusungu kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuwauwa wahalifu na badala yake wawafikishe katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.