Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya NMB, Juma Kimori akimkabidhi Tuzo iliyoitambua benki ya NMB kuwa Benki Salama zaidi Tanzania kwa mwaka 2021 Kaimu Afisa Mkuu Udhibiti na Utekelezaji wa Benki ya NMB, Oscar Nyirenda. Tuzo hiyo imetolewa na Jarida la Glob Finance la nchini Marekani. Kulia ni Mkuu wa Idara ya wateja maalum, Getrude Mallya na mwisho kushoto ni Mkuu wa Idara ya Hazina – Jeremia Lyimo.
Afisa Mkuu wa Fedha wa benki ya NMB, Juma Kimori akionyesha tuzo kutoka jarida la kimataifa la Global Finance lililo itambua benki ya NMB kama Benki Salama zaidi nchini Tanzania. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Wateja Maalum ya NMB, Getrude Mallya na wa kwanza kutoka kushoto ni Kaimu Afisa Mkuu Udhibiti na Utekelezaji NMB, Oscar Nyirenda na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Hazina – Jeremia Lyimo
………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu
NMB ndiyo benki salama zaidi nchini kwa miaka miwili mfululizo baada ya leo kutangaza kupokea tuzo ya ubora huo mwaka huu kutoka jarida la Global Finance la New York Marekani.
Ushindi wa Tuzo ya Benki Salama Zaidi Tanzania ni ushahidi mwingine wa utayari wa NMB kulihudumia taifa, uimara wake kifedha na kuendelea kuongoza sokoni.
Akitangaza mafanikio hayo makubwa, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw Juma Kimori, alisema jarida hilo limewapa heshima hiyo kutokana na kuibuka kinara katika vigezo kadhaa vya kifedha ikiwa ni pamoja na uimara wa mtaji na ukubwa wa mali za benki.
“NMB imetajwa kuwa Benki Salama Zaidi Tanzania 2021 baada ya kuangalia vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na ufanisi na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma jumuishi za kifedha na usalama wa huduma za kimtandao,” Bw. Kimori aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Sababu zingine zilizotufanya kupata tuzo hii ni mapato yatokanayo na mali za benki, kiwango cha amana za wateja, kiwango cha mikopo pamoja na uwiano wa mikopo na amana za wateja. Na katika vigezo vyote hivyo, tumekuwa vinara kwa hapa Tanzania,” kiongozi huyo alitabainisha.
“Kuaminika na kutambulika huku na taasisi kubwa ulimwenguni kama Global Finance kwa mara mbili mfululizo ni fahari kubwa kwetu lakini pia inatuachia changamoto ya kuendelea kujituma katika kuhudumia na kubuni suluhisho zitakazo tufanya tubaki kuwa vinara katika huduma za kifedha hapa nchini,” alisisitiza.
Tuzo za benki salama zaidi duniani hufanyika kila mwaka kwa mabara yote na kwa kila nchi na hutolewa baada ya kufanyika tathmini ya vigezo vya kifedha na kiutendaji.
Bw Kimori alisema ushindi wa NMB unathibitisha uimara na uthabiti wa taasisi hiyo pamoja na mabadiliko ya kidijitali inayoyafanya na uwezo wake kiubunifu katika kuwasaidia wafanyakazi, wateja na jamii kwa ujumla.
“Kuibuka kwetu kidedea kwenye tuzo hizi ni uthibitisho tosha wa hadhi yetu kama benki kinara wa kutengeneza faida na salama zaidi miongoni mwa taasisi za fedha nchini. Hii pia inaimarisha nafasi yetu katika jumuiya ya fedha duniani,” alifafanua.
Hii ni tuzo ya saba ya kimataifa kunyakuliwa na NMB mwaka huu na kufanya jumla ya tuzo ilizoshinda kuwa nane. Tuzo hizo ni pamoja na Tuzo ya Benki Bora nchini kwa mara tisa mfululizo kutoka jarida la EuroMoney.
Mwezi uliopita, kampuni ya Mastercard iliitunuku NMB tuzo maalum kutambua uwekezaji inayofanya kusaidia kupunguza matumizi na kutegemea sana pesa taslimu.
Kwenye taarifa za robo ya tatu ya mwaka 2021, Benki ya NMB ilitangaza kupata faida ya TZS bilioni 211 baada ya kodi na kuendelea kuwa benki kinara wa faida nchini. Kwa sasa thamani ya mali zote za benki hiyo ni zaidi ya TZS trilioni 8.2.
Bw Kimori alisema uwezo huo kifedha unaiweka NMB kwenye nafasi ya kulihudumia taifa vizuri ziadi mwakani na huko mbeleni huku ikendelea kuwa benki kiongozi wa ubunifu na huduma bora kwa wateja.
Kwa mujibu wa mchapishaji na mkurugenzi wa uhariri wa Global Finance, Bw Joseph D. Giarraputo, mwaka uliopita umeonyesha uthabiti wa sekta ya benki iliyosimama imara kusaidia kulikabili janga la virusi vya corona kwa namna tofauti.
“Kwa Tanzania, NMB ni mfano bora wa uimara huo ikiendelea kutoa msaada unaohitajika kwa serikali na jamii katika jitihada za kujikwamua kutokana na athari za kiuchumi za janga hili.”
MWISHO…