…………………………………………………………..
Katika kuelekea sikukuu ya Kristmas na Mwaka Mpya 2022, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya, wageni na wakazi wa mikoa jirani wanasherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.
USALAMA BARABARANI: Kwa kutambua kuwa Mkoa wetu una barabara kuu inayounganisha nchi yetu na nchi jirani pamoja na mikoa jirani, na kwa kuzingatia kuwa ongezeko la vyombo vya moto ndani ya Jiji letu na matumizi makubwa ya vyombo hivyo hasa kipindi cha sikukuu, tumejipanga vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara wakiwemo madereva na watembea kwa miguu.
Tumejipanga kuendelea kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto ili kuangalia usalama wake viwapo barabarani, elimu kwa madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara inaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali. Pia tunaendelea na utaratibu wa kupitisha magari ya abiria na mizigo kwa awamu katika maeneo yenye milima na miteremko mikali kama vile Iwambi, Mlima nyoka na Mwansekwa. Aidha abiria wa mabasi ya mikoa mbalimbali tunaomba waendelee kutuvumilia hasa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu kwa utaratibu wa kuyasindikiza mabasi ya abiria muda wa asubuhi yanapotoka Stendi kuu, lengo ni kupunguza mihemko ya madereva na ajali zisizo kuwa za lazima. Wito wangu kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
MAKANISANI/MISIKITINI: Waumini wa dini ya kikristu na kiislamu hushiriki katika misa, ibada na sala kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba zao, Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha kuwa tunaweka ulinzi na usalama katika makanisa na misikiti. Aidha ninatoa wito kwa viongozi katika makanisa na misikiti kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa ulinzi kwa kutumia kamati za ulinzi na usalama zilizopo misikitini na makanisani ili kuhakikisha ulinzi maeneo ya ndani na nje hasa kwenye maegesho ya magari.
KUMBI ZA STAREHE: Ninatoa rai kwa wamiliki wa kumbi za starehe kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kazi zao hasa kwa kuzingatia leseni zao za biashara zinavyowaelekeza ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kufungua na kufunga sehemu zao za biashara. Pia wenye kumbi za muziki kuhakikisha kumbi zao zinaingiza idadi ya watu inayohitajika ili kuepuka “suffocation”. Aidha nasisitiza wamiliki kuhakikisha wanakuwa na walinzi binafsi ambao wataimarisha ulinzi wa ndani ya kumbi na maeneo ya nje hasa maeneo ya maegesho ya magari.
MAENEO YA BIASHARA: Ulinzi na usalama katika maeneo ya biashara kama vile Masoko makubwa, SIDO, nyumba za kulala wageni na vituo vya mafuta, tumejipanga kuendelea kufanya doria za magari na miguu katika maeneo hayo kwa kushirikiana na walinzi wa makampuni binafsi waliopo maeneo hayo. Ni rai yangu wafanyabiashara kuhakikisha walinzi wanakuwepo na wanafanya kazi yao kwa weledi mkubwa.
FUKWE: Mkoa wetu kwa upande wa wilaya ya Kyela kuna ziwa Nyasa ambapo kuna fukwe kama vile Ngonga, Matema na Kisiba ambazo kwa msimu huu wa sikukuu wazazi, walezi huambatana na watoto na familia zao kwa ajili ya michezo na burudani mbalimbali, tunawataka wamiliki wa fukwe hizo kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri, waangalizi [Guiders] na walinzi binafsi. Jeshi la Polisi litapita maeneo hayo kufanya doria ili kuhakikisha usalama.
ULINZI WA MTOTO: Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa rai kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa watoto, pia kuwasaidia watoto hasa kuwavusha katika maeneo tete kama vile kwenye vivuko vya watembea kwa miguu, maeneo yenye mito ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea. Pia ili kuepuka watoto kupotea katika kipindi cha sikukuu, wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini zaidi katika uangalizi wa watoto wao kila mahali watakapokwenda iwe ni makanisani, misikitini au katika maeneo yenye michezo ya watoto au vivutio vya utalii na fukwe.
MAKAZI: Pia tunasisitiza ulinzi na usalama katika makazi yetu, kuhakikisha kwa wale wanaotoka kwenda kanisani, msikitini na maeneo ya starehe wanaacha waangalizi katika makazi. Pia kuhakikisha tunajilinda kwa kufunga milango na madirisha ili kuepuka uhalifu katika nyumba zetu, ninasisitiza fursa ya ulinzi jirani kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya, “When You See Something, Say Something”.
Pia nitoe rai kwa wenyeviti wa mitaa, watendaji wa Kata na Tarafa kushirikiana na wananchi, vikundi vya ulinzi shirikishi kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao na makazi yao.
Aidha nasisitiza utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kupitia namba za simu zifuatazo:-
RPC…………………………………………………………….0715 009 931
RCO……………………………………………………………0658 376 052
OPERATION OFFICER……………………………………..0765 657 552
RTO…………………………………………………………….0658 376 472
OCD MBEYA………………………………………………….0659 884 996
OCD MBALIZI………………………………………………..0655 248 381
OCD CHUNYA………………………………………………..0659 885 340
OCD MBARALI……………………………………………….0659 885 948
OCD RUNGWE……………………………………………….0659 885 253
OCD KYELA………………………………………………….0659 887 919
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.