*********************
Na John Walter-Babati
Washiriki 9 waliotinga fainali ya shindano la kusaka vipaji vya kuimba muziki wa Injili linaloendeshwa na kituo cha redio cha Smile Fm watapanda jukwaani Desemba 24 mwaka huu siku ya ijumaa katika ukumbi wa Negams Park uliopo mjini Babati bara bara kuu ya kuelekea Singida kupigania nafasi kushinda shilingi laki tano.
Washiriki hao watakuwa na kibarua kigumu cha kuwavutia majaji wabobezi katika tasnia ya muziki ili waweze kuchaguliwa na kula zawadi nono ya fedha Taslimu kwa washindi wa kwanza wa pili na wa tatu.
Washiriki hao walio fanikiwa kutinga fainali ni Rhoda Thomas, Agatha,Philipo John, Vailethi Franki, Ezekieli Rafaeli, Upendo Joseph, Ezekieli Ally, Dorcas Paul na Michaeli Mbarikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Smile Fm Jeston Kihwelo amesema mchakato wa kuwapata washiriki hao waliotinga hatua ya fainali lilikuwa ni ngumu kwani washiriki takribani 19 walijitokeza na wengi wameonyesha vipaji vya hali ya juu.
Amesema mashindano hayo ya Smile Gospel Search yaliyondaliwa na kituo cha redio cha Smile Fm kilichopo mjini Babati mkoani Manyara yamelenga kuibua vipaji vya kuimba nyimbo za Injili mkoani hapo na Tanzania kwa ujumla ambapo amewasihi waliofanikiwa kuingia katika fainali kujipanga vizuri kwa kuwa mchuano ni mkali.
Mratibu msaidizi wa Mashindano hayo Lucas Mondu amewakaribisha watu wa rika zote kuhudhuria katika fainali hizo zitakazofanyika siku ya Desemba 24,2021 katika viwanja vya Negams Park mjini Babati kuanzia saa 10 jioni.
kiingilio katika mashindano hayo ya fainali imepangwa kuwa ni shilingi 5,000 kwa watu wote.
Ikumbukwe kuwa kituo hicho cha redio kinachoongozwa na kauli mbiu Sauti yako,Chaguo lako kimekuwa na utaratibu wa kuanzisha mashindano mbalimbali kwa lengo la kuinua vipaji vya uimbaji na michezo kama serikali inavyosisitiza kupitia wizara ya Utamaduni,sanaa na Michezo.