Meneja wa RUWASA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Boaz Matundali akisaini moja ya mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji kati ya RUWASA na wakandarasi leo mjini Sumbawanga.
Mwakilishi wa kampuni ya Kiluswa Building Contrators ya Sumbawanga akisaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji utakaotekelezwa kijiji cha Msanda Muungano wilaya ya Sumbawanga kwa gharama ya shilingi Milioni 295. Kulia kwake ni Meneja wa RUWASA Rukwa Mhandisi Boaz Matundali akishuhudia.
……………………………………………….
Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji mkoani Rukwa wametakiwa kuwa waadilifu na wazalendo ili wananchi wapate maji vijijini na mijini kwa ustawi wa jamii hatua itakayo ondoa kero za ukosefu wa maji.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati aliposhuhudia hafla ya utiaji saini mikataba minne ya miradi ya maji kwa kati ya Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na wakandarasi mjini Sumbawanga.
“Miradi hii haihitaji stori, tunahitaji siku 180 za mkataba zitumike kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji huku tukizingatia matumizi sahihi ya fedha pamoja na uadilifu “alisema Mkirikiti.
Katika hafla hiyo mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya shilingi 1,383,238,518 itakayotekelezwa kwa siku 180 katika wilaya za Nkasi na Sumbawanga.
Akitoa taarifa kabla ya utiaji saini, Meneja wa Mkoa wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Boaz Matundali alisema jumla ya miradi 19 imetangazwa katika mwaka huu wa fedha ambapo minne kati yake imepata wakandarasi.
Mhandisi Boaz alitaja miradi itakayosainiwa kuwa ni ujenzi wa mradi wa maji Msanda Muungano wilaya ya Sumbawanga wenye thamani ya shilingi Milioni 295.7 chini ya mkandarasi Kiluswa Building Contrators ya Sumbawanga.
Miradi mengine itatekelezwa katika wilaya ya Nkasi ambayo ni ujenzi wa mradi wa maji Lyazumbi (shilingi Milioni 308.4), ujenzi wa mradi wa maji Kacheche (shilingi Milioni 385.0) na mradi wa maji Masolo (shilingi Milioni 395.9) yote itatekelezwa na mkandarasi Consel Construction and Engineering Services ya Mwanza.
Katika hatua nyingine Mhandisi Boaz alisema katika mwaka huu RUWASA mkoa wa Rukwa unatumia wakandarasi katika kutekeleza miradi yake tofauti na ilivyokuwa mwaka uliopita ambapo miradi ilitumia force account na nguvu za wananchi hivyo wanategemea itakamilika ndani ya kipindi cha siku 180 za mkataba.
“Kukamilika kwa miradi hii minne kutasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji maji mkoa wa Rukwa toka asilimia 64 za sasa hadi kufikia asilimia 67 kwenye vijiji “alisisitiza Mhandisi Boaz.
Kwa upande wake mwakilishi wa wakandarasi Anyosisye Kiluswa aliishukuru serikali kwa kutoa kazi hizo kwa wakandarasi wazawa hatua itakayosaidia kukuza biashara na kuchangia upatikanaji ajira.
Kiluswa alitoa ahadi kuwa miradi hiyo wataitekeleza kwa ufanisi na ubora ili kuwezesha wananchi kupata maji kama serikali ilivyokusudia.
Naye Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Thomas Msuta alisema wanafuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inakuwepo kwenye miradi hiyo.
“Sisi TAKUKURU tutafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii ili fedha za serikali zitumike kwa usahihi kuhakikisha lengo la kuwezesha wananchi kupata maji “alisisitiza Msuta.
Mwisho.
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
SUMBAWANGA
21.12.2021