………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WAKANDARASI 17 wa maji ,wameingia mkataba mkoani Pwani kutekeleza miradi yenye thamani ya sh.bilioni 7.8 itakayohudumia watu zaidi ya 45,000 itakapokamilika.
Baada ya hatua hiyo ,wakandarasi hao wameaswa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo ndani ya miezi sita.
Hafla hiyo fupi ya utiaji saini wa mikataba kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa iliyofanyika Mjini Kibaha ,ambapo mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge aliwakumbusha wakandarasi hao kuzingatia muda wa utekelezaji miradi hiyo miezi sita.
“Wakandarasi nyie mmekubalika na mmekidhi vigezo mnapaswa kukamilisha miradi hii kwa wakati kwani Jografia mmnaijua hatutapenda kuona kuna sababu labda zile za majanga kwani mvua siyo sababu hilo hatutalisikiliza,”
“Wananchi wanachohitaji ni maji na siyo vinginevyo na nitafurahi mkinikaribisha kufungua maji yanayotoka siyo kuangalia ujenzi wa kisima na pia mzingatie kuwa Pwani ni mkoa wa uwekezaji wa viwanda hivyo lazima maji ya uhakika,”alisema Kunenge.
Kunenge alieleza ,serikali inajitahidi kutoa fedha kwa ajili ya kupunguza ama kuondoa changamoto ya maji kwa jamii.
Alisema , fedha zilizotolewa kwenye bajeti ya mwaka 2021 serikali ilitoa fedha kiasi cha sh.bilioni 12 sawa na asilimia 41 na zimeongezeka kufikia bilioni 21 sawa na asilimia 76 kwa bajeti ya mwaka 2022 hali ambayo itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwenye mkoa.
Aidha alisema ,wakandarasi wote ni wazalendo hivyo lazima waonyeshe uzalendo na kutumia taaluma yao ili uzalendo wa nchi yao uonekane na mkoa utatoa ushirikiano na wanunue vifaa vinavyotengenezwa hapa nchi vyenye ubora.
Akielezea ju ya miradi hiyo 17 meneja wa RUWASA mkoa wa Pwani Mhandisi Beatrice Kasimbazi alisema kuwa miradi hiyo ni ya awamu kwanza na itatekelezwa kwenye Halmashauri za wilaya zote za mkoa wa Pwani.
Kasimbazi alisema kuwa kupitia miradi hiyo fedha zake zinatokana na Mpango wa maendeleo wa ustawi wa Taifa wa mapambano dhidi ya Covid-19 kiasi cha shilingi bilioni 2.6 Mango wa malipo kwa Matokeo (PbR) 445.4 na Mfuko wa maji bilioni 4.7.
Alisema kuwa bajeti kuu ya mkoa kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ulitengewa kiasi cha shilingi bilioni 21.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Vijijini.
Kasimbazi alisema kuwa fedha hizo zimetokana na Mapambano dhidi ya Covid -19 bilioni 3.7 Mfuko wa maji (NWF) na serikali kuu bilioni 15.2 na Malipo kwa Matokeo (PbR) bilioni 2.4 na ikikamilika itawafikia wakazi 102,307.
Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno alisema kuwa watahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kwa kuitembelea ili kuona mwenendo wake ili kuwapunguzia kero za maji wananchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Pwani Muharami Mkenge alibainisha, upatikanaji wa fedha hizo zitasaidia kukabiliana na changamoto za maji kwenye mkoa huo.
Alifafanua, kuna baadhi ya maeneo maji hakuna hivyo wao kwa kushirikiana na wananchi wataisimamia vema miradi hiyo.