………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Babati
SAFARI ya mwisho ya Baba mzazi wa Mbunge wa vyuo vikuu Dkt Paulina Nahato, marehemu Mchungaji Daniel Nahato imehitimishwa nyumbani kwake Kata ya Bonga Mjini Babati Mkoani Manyara.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na maaskofu wawili, wachungaji 20, viongozi wa serikali na wa CCM na wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Dar es salaam.
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Kaskazini Mashariki, Mussa Nzumbi akizungumza kwenye mazishi hayo amewataka ndugu hao washirikiane ipasavyo kwenye msiba huo.
“Baba wa familia anapofariki dunia, baadhi ya ndugu huwa wanagombana ila ninyi mshikamane mpendane ili maisha mengine yaendelee” amesema Askofu Nzumbi.
Hata hivyo, amewatia moyo wafiwa na waombolezaji wote wakiwemo mke mjane wa marehemu, watoto na kuwataka wamtegemee Mungu katika kipindi hiki kigumu kwao kwa kumpoteza baba yao.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania, Peter Konki, amesema enzi za uhai wake mchungaji Nahato walikuwa marafiki na walikuwa wanawasiliana na kusalimiana mara kwa mara.
“Tulikuwa tunazungumza mara kwa mara juu ya kumtumikia Mungu na hata alipokuwa anatumikia mkoa wa Kilimanjaro kwenye uinjilishaji tulikuwa tunawasiliana,” amesema Askofu Mkuu Konki.
Mbunge wa vyuo vikuu Dk Paulina Nahato amewashukuru viongozi wote na wananchi waliofika kwenye mazishi ya baba yake marehemu mchungaji Nahato.
“Tunawashukuru kwa kutufariji jamani kuanzia hapa Bonga, Babati, Manyara na Tanzania kwa ujumla, asanteni sana kwa kutukimbilia kwenye msiba huu mzito wa marehemu baba yetu,” amesema Dk Nahato.
Mtoto mwingine wa mchungaji huyo Ashery Nahato akisoma historia ya marehemu Mchungaji Nahato amesema alizaliwa mwaka 1940 na kufariki mwaka huu.
Ashery alisema marehemu mchungaji Nahato alijaliwa kupata watoto wanne ila mmoja alifariki dunia hivyo ameacha watoto watatu na mjane.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti na mbunge wa Jimbo la Babati vijijini, Daniel Sillo ametoa pole na rambirambi kwa niaba ya wabunge wote.
Katibu wa CCM wa mkoa wa Manyara, Naomi Kapambala, aliwasilisha pole na rambirambi na kusema chama hicho kipo pamoja na familia hiyo kwenye msiba huo.