Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi wakuu wa kanisa la Wabaptist Tanzania wakiongozwa na Askofu Mkuu Anorld Manase Molel, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Desemba 21,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea zawadi ya Biblia Takatifu kutoka kwa Askofu Mkuu wa kanisa la Wabaptist Tanzania Anorld Manase Molel, mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Desemba 21,2021.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa kanisa la Wabaptist Tanzania wakiongozwa na Askofu Mkuu Anorld Manase Molel (wa pili kutoka kulia kwa Makamu wa Rais ) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Desemba 21,2021
PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS.
***********************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 21 desemba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa kanisa la Wabaptist Tanzania wakiongozwa na Askofu Mkuu Anorld Manase Molel, mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amewashukuru viongozi pamoja na waumini wote wa kanisa hilo kwa kuendelea kuliombea taifa katika kudumisha amani, umoja na mshikamano. Amesema jamii yeyote yenye maadili mema na uzalendo inatokana na mchango mkubwa unaotolewa na viongozi wa dini hapa nchini.
Amesema kanisa la Baptist limekuwa na mchango mkubwa katika kushirikiana na serikali kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya hivyo amewaasa viongozi hao kuendelea kutoa huduma hizo ikiwemo kufungua upya chuo kikuu walichokuwa wanakimiliki hapo awali cha Mount Meru.
Amewasihi viongozi hao wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali ili kutenda yale yalio mema na kumtanguliza Mungu katika utumishi wao. Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha wananchi kutumia mvua zinazopatikana kufanya kilimo cha muda mfupi ili kujipatia mazao ya chakula na biashara.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Anorld Manase ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa makanisa yote hapa nchini na kuahidi kanisa la Wabaptist Tanzania litaendelea kuliombea taifa ili kuwepo Amani na mshikamano. Ameiomba serikali kusimamia kikamilifu misamaha ya kodi inayotolewa kwa makanisa wakati wa kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za elimu na Afya.
Viongozi hao wa kanisa la Wabaptist Tanzania wameiomba serikali kupitia upya sheria za usajili wa jumuiya za kidini hapa nchini ili kulinda misingi iliowekwa kutoharibiwa kutokana na kuongezeka kwa huduma hizo hapa nchini.
Aidha wamesema katika kuliletea taifa maendeleo wanaunga mkono suala la sensa ya watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 na kuiomba serikali kuongeza kasi katika utoaji elimu ya sensa hiyo ili wananchi wote watambue umuhimu wake.
Katika hatua nyingine viongozi hao wa dini wameiomba serikali kuweka mkazo katika masomo yanayowafanya wahitimu kujitegemea ikiwemo masomo ya kilimo na biashara ili kuwawezesha kutotegemea kuajiriwa pindi wanapohitimu masomo yao.
Makamu wa Rais amewahakikishia viongozi hao wa dini kwamba serikali itaendelea kupokea ushauri na maoni kutoka katika taasisi za dini na kuahidi changamoto zote walizozitoa kanisa la Wabaptist Tanzania serikali ya awamu ya sita itazifanyia kazi.