**************************
Na John Walter-Iringa
Wanamichezo wa Chuo Cha Serikali za Mitaa (LGTI) walioshiriki michezo ya 46 ya Shirikisho la Michezo la Vyuo vya elimu ya juu Tanzania (SHIMIVUTA) wamefanya vizuri katika michezo mbalimbali inayoandaliwa na Shirikisho hilo kila mwaka.
Mashindano hayo ambayo yalifikia kilele mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohamed Moyo.
Akitoa hutoba yake kwa waratibu, washiriki na wananchi mbalimbali waliohudhuria mashindano hayo Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Moyo aliwapongeza kwa kufanya mashindano hayo huku akiwaomba waandaji hao kwa mwaka 2022 yafanyike tena mkoani humo.
Alisema kuwepo kwa mashindano hayo kumeufanya mkoa wa Iringa kuchangamka kwa shughuli za michezo na kiuchumi na pia kumetoa fursa kwa vyuo mbalimbali kujitangaza hasa katika ukanda wa nyanda za juu kusini.
“Ndugu waandaji na washiriki wote wa michezo ya SHIMIVUTA mwaka 2021 nna uhakika kwa kukaa kwenu katika mkoa wa Iringa kwa kipindi cha Zaidi ya wiki mmekuwa salama na mmefurahia mazingira ya mkoa wa Iringa na pia mmepata fursa ya kujitangaza na kuwahamasisha vijana wetu wenye nia ya kupata elimu kuja kujiunga na vyuo vyenu kwani leo hii wamejionea jinsi Tanzania ilivyokuwa na idadi kubwa ya vyuo na kujua kuwa vyuoni mbali masomo mbalimbali yanayofundishwa kumbe pia kuna fursa ya kushiriki katika michezo kwani kwa sasa michezo ni ajira, ningetamani na mwaka 2022 mashindano haya yafanyike tena mkoani Iringa” Alisema Mhe. Moyo.
Akitangaza zawadi mbalimbali zilizoshindaniwa tangu mwanzo wa mashindano hayo Mjumbe wa kamati tendaji wa michezo ya SHIMIVUTA ambaye pia ni Mwalimu wa michezo kutoka Chuo Cha Serikali za Mitaa, Ashraf Athumani alisema kwa mwaka 2021 LGTI imefanya vizuri ukilinganisha na mashindano yaliyopita kwa kuwa mwaka huu LGTI ndio chuo pekee kilichochukua ushindi wa jumla katika Mchezo miwili ambayo ni riadha na mpira wa pete (Netball) ukilinganisha na vyuo vingine vilivyochukuwa ushindi wa jumla kwa mchezo mmoja mmoja.
Mwalimu huyo wa michezo alisema kwa mwaka huu kuna baadhi ya vyuo havikushiriki lakini mwakani watajitahidi kupeleka mialiko mapema ili ile dhana ya vyuo vya elimu ya juu ionekane kwa kila Chuo kushiriki.
“Tangu tarehe 9/12 mashindano yalivyoanza mpaka leo tarehe 18 mashindano yamekuwa ya mafanikio sana na wanamichezo wote wameonesha uwezo wao kwa kushiriki katika michezo mbalimbali na hatimaye mabingwa wamepatikana na sisi kama waratibu tutajitahidi kuhakikisha mwakani vyuo vingi vinashiriki ili kuongeza hamasa na ushindani” Alisema bwana Ashraf.
Nao wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wamefurahishwa na mashindano hayo na kusema pamoja na kushiriki michezo lakini pia kumewapa fursa ya kubadilisha mazingira na kuongeza marafiki kutoka vyuo tofauti vilivyoshiriki.
“Tumefurahi kuja Iringa na kushiriki mashindano haya ya SHIMIVUTA na tunaomba mwakani waandaji waalike vyuo vingi ili ushindani uwepo” Alisena Abdulrahman Shekh Abdallah Mwanafunzi kutoka Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT)
Kwa upande wao Teresia Nicolaus Umuri aliyeshinda nishani (medali) nne za dhahabu katika riadha na Suzana Japhet nahodha wa mchezo wa pete (Netball) kutoka Chuo Cha Serikali za Mitaa wameeleza furaha yao kwa kushiriki na kushinda nafasi ya kwanza katika michezo hiyo na kuahidi kutetea nafasi zao katika mashindano ya mwakani.
Katika mashindano ya mwaka huu mabingwa katika mchezo wa mpira wa miguu ni Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT),mshindi wa pili ni Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) na Mshindi wa Tatu ni Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Mpira wa pete (Netball) Mshindi wa kwanza ni Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), mshindi wa pili ni Chuo Cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) na mshindi wa tatu ni Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) katika mpira wa kikapu mshindi wa kwanza ni Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE), mshindi wa pili ni Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na mshindi wa tatu ni chuo Cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) kwa upande wa mpira wa wavu wanaume mshindi wa kwanza ni Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), mshindi wa pili ni Taasisi ya Teknolojia Dar es salam (DIT) na mshindi wa tatu ni Taasisi ya Uhasibu Arusha (AIA) na mpira wa wavu wanawake mshindi ni wa kwanza ni Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, mshindi wa pili ni Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA) na mshindi wa tatu ni Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT).
Mashindano hayo vilevile yameshuhudiwa zikitolewa nishani (medali) mbalimbali kwa washindi wa riadha kuanzia mita 100 hadi mita 1500 na mbio za kupokezana vijiti, wachezaji bora katika michezo yote na vyeti vya ushiriki kwa kila Chuo.
Mwaka huu 2021 mashindano ya SHIMIVUTA yameshirikisha vyuo 14 ambavyo ni Chuo Cha Serikali za Mitaa (LGTI), Kituo Cha Mahusiano ya Nje (CFR),Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam(DIT),Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE),Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT),Chuo Cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP),Chuo Cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA),Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA),Chuo Cha Maji (WI), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Taasisi ya Ustawi wa Jamii na kwa mwaka 2022 mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza.