Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akiangalia mtambo uliokuwa ukitumika kutengenezea seal za plastiki zilizopigwa marufuku kutokana na kuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira alipotembelea kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji ya Afya kilichopo Kisarawe II Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akipata maelezo kuhusu uwekeaji wa mihuri mbadala wa seal za plastiki kutoka kwa Bw. William Mhavila kutoka kitengo za uzalishaji alipotembelea kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji ya Afya kilichopo Kisarawe II Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akisikiliza maelezo kuhusu mfumo wa majitaka uliorekebishwa kutoka kwa Bi. Zhang Ping, Meneja wa kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kinachojihusisha na urejeleshaji wa plastiki na kuzalisha mabomba.
*************************
Agizo la Serikali la kusitisha utengenezaji na uwekaji wa plastiki laini (seal) kwenye mifuniko ya chupa za maji limeendelea kutekelezwa tangu lilipotolewa Oktoba 11, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo.
Hayo yamebainika leo Desemba 21, 2021 wakati wa ziara ya Waziri Jafo ya kufuatilia maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na Serikali kuhusu utunzaji wa mazingira.
Ametembelea na kukagua kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji ya Afya na cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kinachojihusha na urejelezaji plastiki na kuzalisha mabomba vilivyopo eneo la Kisarawe II katika Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Alisema Serikali ilitoa maelekezo hayo kutokana na seal hiyo haiwezi kurejelezeka na inachafua mazingira pindi inapotupwa na kuzagaa ovyo hali inayoweza kusababisha vifo vya mifugo na samaki baharini wanapomeza.
Waziri huyo alibainisha kuwa pamoja na maelekezo hayo ya Serikali bado kuna baadhi ya kampuni bado hazijatekeleza huku akisisitiza kuwa ifikapo tarehe ya mwisho ya marufuku hiyo maji yatakaendelea kuwekewa seal hiyo yatapigwa marufuku sokoni.
Aidha, aliwatoa wasiwasi wananchi wanaodhani kuwa bila matumizi ya viplastiki hivyo kuna uwezekano wa maji kuchakachuliwa akisema kuwa matumizi ya mhuri wa moto unasaidia kuondoa changamoto hiyo.
“Nimekuja hapa kwenye kiwanda hiki cha maji na nimefarijika sana kuona tayari wameshaanza kutekeleza agizo hilo hawaweki tena viplastiki vile na wanatumia mtambo maalumu wa kuweka stamp (mhuri) na huyu ametambua umuhimu wakupila kodi kwa hiyo huwezi kununua maji hayo hadi yawe na mhuri huo,” alisema.
Kwa upande wake Bw. William Mhavila kutoka kitengo cha uzalishaji cha kampuni hiyo alisema hivi sasa wanatekeleza agizo la Serikali kwa kusisitisa uzalishaji wa vifuko hivyo.
“Kama mnavyoona tumezima mtambo huu uliokuwa unazalisha zile seal za plastiki na hivyo tumeanza kutekeleza agizo la Serikali ili tuweze kutunza mazingira,” alisema Mhavila.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo alifanya ziara katika kiwanda cha Tanzania Ruidar Co. Ltd kinachojihusisha na urejeleshaji wa plastiki na kuzalisha mabomba.
Akiwa kiwandani hapo alionesha kuridhishwa na utekelezaji wa agizo lake la miezi mitatu kwa kampuni hiyo la kurekebisha mfumo wa uchujaji wa majitaka ambao ulitiririsha majitaka kwenye makazi ya watu.
Waziri Jafo alisema kuwa kiwanda hicho kimetekeleza agizo hilo kwa asilimia mia moja na kuwataka wengine waige mfano huo kwa mustakabali wa kulinda mazingira yetu.
Pia alielekeza maafisa mazingira kufuatilia viwanda mbalimbai katika eneo hilo la Kigamboni kuona namna gani wanatimiza matakwa ya kisheria katika suala zima la utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake Meneja wa kiwanda hicho, Bi. Zhang Ping alisema kutokana na hatua hiyo hivi sasa anarejeleza majitaka tofauti na awali alikuwa akinunua mara kwa mara hivyo kupunguza gharama.