Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara Mhandisi Vitalis Bilauri, wakati akikikagua Kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma za usafiri kati ya Mwigobero Wilayani Musoma na Kinesi Wilayani Rorya, ambapo amewahidi wananchi kuleta kivuko kingine hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akipitia taarifa za mahudhurio katika Kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma za usafiri kati ya Mwigobero Wilayani Musoma na Kinesi Wilayani Rorya, mkoani Mara
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoka kukagua Kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma za usafiri kati ya Mwigobero Wilayani Musoma na Kinesi Wilayani Rorya, mkoani Mara. Kivuko hichi hivi karibuni kitapelekwa kwa ajili ya matengenezo makubwa.
Muonekano wa Kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma za usafiri kati ya Mwigobero Wilayani Musoma na Kinesi Wilayani Rorya, mkoani Mara. Kivuko hicho kinatarajiwa kufanyiwa matengenezo makubwa hivi karibuni.
PICHA NA WUU
**********************
Serikali imeahidi kupeleka Kivuko kingine ili kuruhusu Kivuko cha MV. Musoma kinachotoa huduma za usafiri kati ya Mwigobero Wilayani Musoma na Kinesi Wilayani Rorya, kufanyiwa marekebisho makubwa.
Hayo yamesemwa mkoani Mara na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akikagua kivuko hicho ambacho ni cha muda mrefu na sasa kimekuwa na changamoto nyingi kwa watumiaji ikiwemo kutofanya kaza mara kwa mara na kuwa na mwendo mdogo.
“Kivuko hiki lazima kipelekwe kutengenezwa na hatuwezi kutoa hikiwakati hapa hakuna kivuko kingine mbadala hivyo muda si mrefu kivuko kingine kitaletwa kuendelea kutoa huduma hapa ili hiki kikikafanyiwa marekebisho”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuweka utaratibu mzuri unaoleweka wa ukaguzi wa vivuko vyote hapa nchini.
“Nimekagua vitabu vyote vya ukaguzi na hakuna maelezo yoyote yanayoonesha nini kimekaguliwa katika kivuko hichi cha kufanyia marekebisho hatutaki makosa ya zamani yajirudie”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesisitisha ujenzi wa jengo la abiria na huduma za vyoo kwa ajili ya abiria wa Kivuko hicho ambalo linajengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 86 na kutoridhishwa na jengo hilo ambalo halina thamani ya fedha hizo kuagiza apelekewe makadirio mapya ya ujenzi huo.
“Fedha ya Serikali haiwezi kupigwa namna hiyo tupo hapa kwa ajili ya kusimamia kazi ziendelee hivyo nitaleta hapa watalaaam wapitie upya na wale wote waliohusika na ujenzi wa jengo hili watachukuliwa hatua za kisheria”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoa wa Mara Mhandisi Vitalis Bilauri, amemueleza Waziri huyo kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kubeba tani 85 na abiria 330 ambapo kwa sasa kinahitaji marekebisho makubwa kwani kimekuwa kikileta changamoto.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Halfan Haule, amemueleza umuhimu wa kivuko hicho cha mbadala kufika katika eneo hilo kwa kuwa wananchi wa wilaya hizi mbili wanautumia sana usafiri wa Kivuko ambapo hiki cha sasa wanatumia muda wa dakika 45.
Vilevile, Mwananchi wa Mwigobero Bw. Athuman Mageza, amemuomba Waziri huyo kuleta Kivuko kilichofunikwa juu kwa ajili ya kujikinga kipindi cha mvua na jua kali.