*************
JOHN MAPEPELE–WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa mikoa yote nchini kuiga Mkoa wa Mbeya katika kushirikiana na Wizara yake kuandaa Tuzo za Filamu katika miaka ijayo ili kukuza vipaji na kutoa ajira kwa wasanii wengi zaidi walio kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini.
Mhe. Bashungwa ametoa kauli hiyo Jijini Mbeya katika kilele cha utoaji wa Tuzo za Filamu nchini iliyoratibiwa na Bodi ya Filamu chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Disemba 18, 2021. Mchakato wa kutafuta filamu hizo bora umechukua zaidi ya miezi mitatu.
“Ndugu yangu Comrade Juma Zuberi Homera, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakupongeza sana kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu chini ya usimamizi wa wizara yangu.”amesisitiza Mhe. Bashungwa
Mhe. Bashungwa amesema kufanyika kwa tamasha hili la kwanza katika historia ya Tanzania kabla na baada ya uhuru ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kushirikisha wadau, kurejesha utamaduni wa kutoa tuzo kwa wadau wa sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo hapa nchini.
Aidha amesema Serikali imeshatenga kiasi cha bilioni 1.5 kwenye mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni kwa ajili kukuza na kuendeleza shughuli za Utamaduni na Sanaa ikiwa ni pamoja na Filamu.
“Ninawajulisha kuwa tuzo hizi ni endelevu, hivyo ninawakaribisha wadau wote wenye nia ya kushirikiana na Serikali kwa mwaka 2022.” Amehimiza Mhe. Bashungwa.
Pia aliipongeza Bodi ya Filamu kwa ubunifu huu ambao umeonesha dira ya Serikali katika kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa nchini.
Waziri Bashungwa ameongeza kutokana na umuhimu na mapenzi yake kwenye tasnia ya filamu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan pamoja na majukumu mengi aliyonayo ameandaa filamu ya Royal Tour ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuitangaza taswira ya Tanzania na kuvutia watalii na wawekezaji nchini.
Katika Kilele hicho Rais Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo ya heshima kwa mchango wake katika tasnia ya filamu nchini tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba yake na Mhe. Innocent Bashungwa huku Mhe. Bashungwa na Naibu wake Bi Pauline Gekul wakipokea tuzo na wasanii 30 kunyakua tuzo za filamu nchini.
Hafla ya kilele cha Tuzo za Filamu nchini imehudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali akiwamo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt.Tulia Akson ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Zuberi Homera, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi,Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Dkt. Angelina Lutambi na viongozi kadhaa wa mikoa ya Mbeya na mikoa jirani, na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Injinia Maryprisca Mahundi.