Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka,wakati akitoa taarifa ya Kikao cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi CCM kwa wandishi wa habari kilichofanyika leo Desemba 18,2021 jijini Dodoma.
Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya Kikao cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi CCM kilichofanyika leo Desemba 18,2021 jijini Dodoma.
………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, Dodoma
Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi(NEC), imepokea na kuidhinisha maandalizi ya maadhimisho ya miaka 45 ya CCM ambayo yatazinduliwa Januari 29, mwaka 2022 Mkoa wa Kusini Unguja.
Pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa ustawi wa wananchi wote.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kikao cha Halmashauri hiyo kilichoketi jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti, Rais Samia.
Amesema kikao kimeidhinisha maadhimisho yataanza Januari 23, mwaka 2022 na yatazinduliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein Januari 29.
Amebainisha kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Mkoa wa Mara ambapo Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia atakuwa mgeni rasmi.
“Katika madhimisho haya ya kuzaliwa kwa Chama cha CCM yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo matembezi ya mshikamano na kutafakari uchaguzi wa ndani ya chama ambao unatarajiwa kufanyika mwakani pamoja na kutafakari azimio la Arusha linalosisitiza uongozi bora na siasa safi,”amesema
Katika hatua nyingine hatma ya wabunge Humphrey Polepole, mbunge wa Ukonga Jerry Slaa pamoja na Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima iko mikononi mwa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa baada ya taarifa ya kamati ya maadili ya wabunge kutua mbele ya kamati hiyo.
Shaka,amesema wabunge hao wote watatu wataitwa kwenye Kamati kuu ya chama hicho Taifa ili kupatiwa haki yao ya msingi na kikatiba ya kusikilizwa.
“Tayari taarifa ya kamati ya maadili ya wabunge wa chama cha Mapinduzi na ile ya Bunge ipo kamati kuu na wabunge hawa watatu wataitwa ili kupatiwa haki yao ya msingi ya kujieleza katika siku ambayo itapagwa na kamati kuu ya CCM ”amesema Shaka