Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa agizo kwa wahandisi wa maji chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) nchini kuhakikisha wanatumia taaluma zao kuwezesha wananchi kupata maji ya uhakika karibu na makazi yao.
Ametoa agizo hilo leo (17.12.2021) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa pamoja na watumishi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini pamoja na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Rukwa kukagua miradi ya maji.
Waziri Aweso alisema mkoa wa Rukwa unavyo vyanzo vingi vya maji hivyo hakuna sababu ya kwanini wananchi wasipate maji wakati serikali ya Awamu ya Sita inatoa fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“Kipimo cha Mhandisi wa maji ni watu kupata maji ya uhakika. Michakato isiyokuwa na ulazima tuachane nayo twendeni tukatekeleze miradi ya maji vijijini kwa spidi. Tutapimana kwa kigezo hiki kote nchini” alisema Aweso.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso ametoa agizo kwa wahandisi wa maji kote nchini kuwa katika kuadhimisha Wiki ya Maji tarehe 22 Machi mwaka ujao kila wilaya lazima izindue miradi ya maji kwa kuwa bajeti ipo.
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa, Aweso amewataka kufanya kazi kwa karibu na RUWASA ikiwemo kupata taarifa za utekelezaji miradi na kufuatilia ubora wake ili wananchi wanufaike na fedha za serikali.
“Viongozi wa mkoa mnayo nafasi ya kusimamia na kufuatilia na kujua taarifa za RUWASA .Kusiwepo usiri na jamii ishirikishwe ili lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kumtua ndoo kichwani mama litimie kote nchini” alisisitiza Waziri Aweso.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA mkoa wa Rukwa Mhandisi Pius Boaz amesema wakala unaendelea kutekeleza miradi kwa kufikisha maji vijijini ambapo katika mwaka huu wa fedha jumla ya miradi Hamsini inaendelea kutekelezwa kote mkoani Rukwa.
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo linalosimamiwa na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) hadi kufikia mwezi Novemba ni asilimia 63. Huduma hii inapatikana kupitia visima vifupi, visima virefu vyenye pampu za mkono, skimu za maji ya mtiririko, miradi ya kusukuma kwa mashine na chemichemi.
Mhandisi Boaz alibainisha kuwa idadi ya vijiji 339 mkoa wa Rukwa vinavyopata ni 201 na visivyopata huduma ya maji ni 138 ambapo RUWASA imejiwekea Mpango wa Miaka mitatu (3) kuanzia mwaka 2020/2021 – 2023/2024 kuhakikisha kuwa vijiji vyote 147 visivyo na huduma ya Maji vinapata huduma hiyo muhimu.
Waziri Aweso amezindua miradi ya maji ya kijiji cha Kizungu wilaya ya Sumbawanga, mradi wa maji kijiji cha Sopa na Katete Wilaya ya Kalambo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kalambo Josephat Kandege aliyeshirikikwenye ziara ya Waziri huyo wa maji akizungumza kwenye kijiji cha Sopa aliwasihi wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili yaendelee kupatikana miaka mingi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya RUWASA mkoa wa Rukwa imeonyesha kuwa mahitaji ya maji katika Mkoa wa Rukwa yanakadiriwa kufikia lita 31,981,750 kwa siku ambapo katika maeneo ya vijijini ni lita 26,366,700 kwa siku na kwa Miji midogo ya Laela, Namanyere, Matai mahitaji ni lita 5,615,050 kwa siku.
Waziri Aweso kesho ataendelea na ziara yake wilayani Nkasi kuzindua miradi na kuzungumzia na wananchi.