Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima akikagua gwaride maalum la wahitinu wakati wa kufunga kozi ya Uongozi ya Kijeshi kwa Maafisa wa ngazi mbalimbali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Chuo cha Jeshi hilo kilichopo Chogo, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima (katikati), akikagua Bweni jipya lenye uwezo wa kubena wanafunzi 100 katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Chogo, Handeni, Mkoani Tanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima (wapili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa wahitimu ambao ni kamati ya ujenzi baada ya kuzindua miradi mbalimbali na kuweka jiwe la msingi wakati wa hafla ya kufunga kozi ya Uongozi ya Kijeshi kwa Maafisa wa ngazi mbalimbali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Chuo cha Jeshi hilo kilichopo Chogo, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wahitimu baada ya kufunga kozi ya Uongozi ya Kijeshi kwa Maafisa wa ngazi mbalimbali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Chuo cha Jeshi hilo kilichopo Chogo, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, leo. Picha na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, MOHA, Handeni.
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kukiendeleza Chuo cha Zimamoto kilichopo Chogo, Wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Kailima pia amepongeza jitihada na juhudi kubwa ambazo wanafunzi wamefanya na kuahidi Wizara itaandaa mikakati mbalimbali Ili kuweza kukiendeleza na kukikuza zaidi chuo hicho kwani tayari juhudi binafsi zimaonekana.
Naibu Katibu Mkuu Kailima amezungumza hayo wakati akifunga mafunzo ya Uongozi ya Kijeshi kwa Maafisa wa ngazi mbali mbali ya Jeshi hilo, Chogo, Wilayani humo, leo.
“Nawapongeza sana kwa jitihada na juhudi kubwa ambazo wanafunzi mmefanya, Wizara itaandaa mikakati mbalimbali Ili kuweza kukiendeleza na kukikuza chuo hicho kwani tayari juhudi binafsi zimaonekana,” alisema Kailima.
Kailima pia alizindua baadhi ya majengo ya Chuo hicho ambacho ni kikubwa na kina miradi mbalimbali ya ujenzi inayoongozwa na Jeshi hilo.
“Pia nampongeza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkuu wa Chuo cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na wasaidizi wake wote kwa kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo katika chuo hiki na kuahidi kuendelea kuishauri Serikali kulisaidia Jeshi hili na kuhakikisha linafikia Malengo yote yaliyopangwa,” alisema Kailima.
Majengo aliyozindua na kuweka jiwe la msingi ni pamoja na Majengo mawili mapya ya mabweni ya wavulana na tanki kubwa la kuhifadhia maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kailima alishangazwa na jitihada za uongozi wa Chuo pamoja na wanafunzi ambao wamekuwa wakipita chuoni hapo Kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitolea kufanya ujenzi wa majengo hayo pasipo kupata fedha toka Serikali kuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Zimamoto na Uokoaji Naibu Kamishna (DCF), Kennedy Komba alisema majengo yote mapya yanayoonekana ni nguvu za wanafunzi ambao wamekuwa wakiendelea kutoa michango kutoka mifukoni mwao, pamoja na jitihada za wadau mbalimbali ambao walichangia vifaa vya ujenzi.
“Ndugu mgeni rasmi katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 na 2021/2022 Chuo cha Zimamoto kimefanikiwa kujenga jumla ya mabweni 9 ambapo mabweni 7 kati yake yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 50 kwa kila bweni, na mabweni mawili yana uwezo wa kuhudumia wanafunzi 100 kwa kila bweni,” Alisema DCF Komba.
Baada ya uzinduzi wa majengo na uwekaji wa mawe ya msingi Naibu Katibu Mkuu ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi, aliwapongeza Maafisa wote 161 waliohitimu kwa uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu kwa kipindi chote walichokuwepo mafunzoni.
*MWISHO*