Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi. Na Dotto Mwaibale, Singida WAKAGUZI wa Dawa na Vifaa Tiba wa Halmashauri za Mkoa wa
Singida wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi na uzalendo ili kulinda afya za
wananchi na waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. Ombi hilo limetolewa na mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida,
Beatus Choaji wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wakaguzi wa Dawa na
Vifaa Tiba wa Halmashauri za Mkoa wa Singida yalioanza leo kwa niaba ya
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) “Nitumie nafasi hii kuwashukuru TMDA kwa kujali afya za
wananchi na kuamua kutoa mafunzo haya mkoani hapa na kukasimisha baadhi ya
majukumu yenu ngazi ya halmashauri lengo likiwa ni kulinda afya za watanzania
ili ni jambo zuri” alisema Choaji. Alisema TMDA ni
Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia
Wazee na Watoto yenye jukumu la kuthibiti ubora, usalama, ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kuwa imeundwa chini ya sheria ya dawa na vifaa
tiba sura namba 219. Alisema majukuku ya TMDA ndiyo yanayo paswa kufanywa na
wakaguzi hao hivyo ni jukumu lao
kuyalinda na si ya kuyapuuzia kwa kuwa wanafanya kazi ya kulinda afya za
wananchi wa Tanzania. Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati TMDA Sonia Mkumbwa
akizungumzia suala zima la ukasimishaji wa baadhi ya madaraka na majukumu
kwenye halmashauri alisema kulitokana na mamlaka aliyopewa Waziri mwenye dhamana ya
Afya chini ya Kifungu cha 121 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219. “TMDA imekasimisha majukumu yake kupitia Kanuni za
Kukasimu baadhi ya Madaraka na Majukumu ya TMDA kwa Halmashauri kupitia GN No.
476 za Mwaka 2015 pamoja na marekebisho yake GN No. 19 ya mwaka 2017″
alisema Mkumbwa. Alisema katika kukasimu majukumu na madaraka hayo, Waziri
amezingatia pia kifungu cha 113(2) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya
Halmashauri za Wilaya [Local Government (District Authorities) Act], Sura 287
na kifungu cha 57(2) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Halmashauri za Miji
[Local Government (Urban Authorities) Act), Sura 288. Aliongeza kuwa lengo kuu la kukasimisha baadhi ya madaraka
na majukumu ya TMDA kwa Halmashauri ni kusogeza karibu na wananchi huduma za
udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Mchunguzi wa dawa kutoka TMDA James Tanguye akizungumzia
maadili na wajibu wa wakaguzi hao alisema wanapaswa kuzingatia Utaalam
(Professionalism),Uaminifu na kutimiza wajibu. Alisema malengo ya mafunzo hayo kwa wakaguzi hao ni kuongeza
uelewa wa wakaguzi kuhusu maadili na wajibu wa wakaguzi kusisitiza umuhimu wa
kuzingatia maadili na kuwakumbusha kufanya kazi kwa ueledi na kutoa maamuzi
sahihi kulingana na Sheria na taratibu za kazi na kuongeza ufanisi katika
utendaji kazi. |