***********************
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo amemuwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Afya wa Nchi za Afrika na Nchi ya Uturuki ulioyafanyika Jijini Istanbul Uturuki.
Mkutano huo wa tatu wa ushirikiano baina ya Uturuki na Nchi za Afrika unafanyika kipindi ambacho Ugonjwa wa UVIKO-19 umekuwa ni changamoto kubwa kwa ulimwengu huku agenja ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo ikichukua sehemu kubwa ya majadiliano katika mkutano huo.
Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya kujikinga pamoja na chanjo bure kwa wananchi.
Dkt. Mollel amesisitiza suala la kuboresha zaidi ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kusaidia zaidi upatikanaji wa chanjo zaidi, mapinduzi ya Sayansi na Tteknolojia yatakayochagiza upatikanajiwa tiba sahihi dhidi ya UVIKO-19 pamoja na magonjwa mengine nyemelezi.
Katika hatua nyingine Dkt Mollel amesifu ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uturuki ambao tunashuhudia madakrari kutoka Uturuki kuja kufanya kambi za kitababu na kubadilishana uzoefu na wataalam (technological transfer) kuhusu masuala ya kitabibu.
Katika kuboresha zaidi mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki, Dkt. Mollel ameiomba Serikali ya Uturuki kufundisha Lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa kada za afya vyuoni ili pindi wanapofika nchini kwa ajili ya mafunzo au kazi waweze kuwasiliana kwa ufanisi zaidi hali kadhalika kwa Watanzania wanaosoma masomo ya kada za afya ano wasome lugha ya kituruki kitu ambacho kitaboresha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.