Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwangomo (kushoto) akimueleza jambo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka (wa kulia) baada ya kuwasili kwenye eno hilo la Hifadhi ya Taifa ya Saadani ambapo kumekuwa na athari za mazingira kutokan na shughuli za uzalishaji Chumvi.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka (wa mbele) akiangalia vyungu vya kuzalishia Chumvi eneo la Buyuni Wilayani Pangani Tanga, wa nyumq ni Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwangomo.
***********************
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesitisha shughuli za mradi wa uchimbaji na uvunaji wa chumvi zinazofanyika katika kijiji cha Buyuni Kitopeni Wilayani Pangani mkoa wa Tanga jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Hayo yamesemwa wilayani Pangani na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Mhandisi Samuel Gwamaka wakati wa ziara ya kukagua eneo hilo, alisema kuwa amesitisha shughuli zote za mradi huo na endapo mwekezaji huyo atakiuka amri hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Alisema wanasimamisha shughuli hizo baada ya kugundua kuwa kimazingira eneo hilo ni nyeti hususani kwa wanyama mbalimbali wakiwemo Tembo wanaotokea hifadhini na kutembea wakati mwingine kupumzika katika eneo hilo.
Pia amesema mradi huo unatishia maisha ya wanyamapori waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani pamoja na kuwepo kwa uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.
Aidha Baraza hilo limemtaka mwekezaji huyo pia kuwathibitishia kama alifanya tathimini ya athari ya mazingira kabla ya kuanza kwa mradi huo na kujua ni athari gani zingeweza kujitokeza pindi wanafanya shughuli za uchimbaji wa matuta( vyungu) vya kuvunia chumvi.
“Kitendo cha mwekezaji huyu kukiuka utaratibu moja kwa moja tunamfungia kufanya shughuli, na ikithibitika huu mradi upo kinyume na sheria, umekiuka taratibu basi tutakwenda kuweka zuio na kumtaka mmiliki wa mradi huo kuyarudisha maeneo hayo kama alivyoyakuta hapo awali,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephrahim Mwangomo alisema eneo ambalo mwekezaji huyo anafanyia shughuli zake ni moja kati ya maeneo muhimu ya mbuga ambayo hutumiwa na tembo kujipatia chakula na kupumzika.
Alisema mwekezaji huyo alipokwenda ofisini kwao walimshauri kubadilisha matumizi eneo hilo kwa kuacha kuchimba chumvi na kufikiria kujenga hoteli kwa ajili ya watalii.
“Hapa Saadani tunapokea watalii 4000 kwa mwaka kutoka nje, wakati wenzetu wa Zanzibar wanapokea watalii 300,000 kwa mawaka na wamesema wanauwezo wa kuhakikisha hao wanaoenda Zanzibar kuja hapa Saadani hivyo tunaweza kupata hata watalii 50,000 na Zaidi lakini changamoto kubwa ni malazi ya kuwalaza Watalii (Hoteli)”
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Buyuni kilichopo kata ya Mkwaja Wilaya ya Pangani, Diwani Waziri alisema, kuwa mradi huo wa uchimbaji chumvi unaomilikiwa na mwekezaji ulioanza mwaka 2015 na alipewa na kijiji heka 50 ili aziendeleze na kufanya maendeleo katika kijiji hicho. Baadaye Mwekezaji aliongezewa hekari nyingine 100 na Wamiliki wengine hvyo kupelekea mpaka sasa kumiliki hekari 150
“Pamoja na kwamba mwekezaji huyu tulimpatia heka 50 ili azitumie kwa shughuli zake, tunakiri kwamba hatukuwashirikisha Hifadhi ya Saadani (SANAPA) wakati wa kufanya maamuzi ya haya mambo,” alisema