Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira NEMC Dkt. Samuel Gwamaka wa kwanza kutoka kulia akiwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Kitaifa kutoka Baraza hilo akizungumza na mmoja wa viongozi wa EACOP walipofanya ziara kwenye mradi wa bomba la mafuta Chongoleani Mkoa wa Tanga kukagua uhifadhi na utunzaji wa mazingira wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Dkt. Samuel Gwamaka wanne kutoka kulia akiwa na wawekezaji na wadau mbalimbali walioshiriki kikao kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwenye mradi wa bomba la mafuta Chongoleani mkoa wa Tanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Dkt. Samuel Gwamaka mwenye suti ya bluu akiwa na viongozi wa Kata ya Chongoleani na wadau wengine wa maingira wakiwa ulipo mradi wa bomba la mafuta alipoenda kukagua utelekelezaji wa Sheria ya maingira katika mradi huo.
Eneo ambalo uwekezaji wa bomba la mafuta unafanyika. NEMC ilifika kwa ajili kuangalia utekelezaji wa Sheria ya mazingira wakati mradi huo ukiwa katika hatua za awali.
****************
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka, amefanya ziara katika eneo linalotarajiwa kujengwa mradi wa kituo kitakachopokea na kuhifadhi mafuta katika Kijiji cha Chongoleani Tanga.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa Sheria, Taratibu na Kanuni za utunzaji wa mazingira katika hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi huo.
Ziara hii ni moja ya utekelezaji wa ajenda kubwa ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Sisi kama NEMC ni lazima tutimize maagizo ya Mhe. Rais na moja ya mikakati ambayo tumeiweka ni kuanza kuwa na mtazamo chanya kwa maana ya kwamba wawekezaji wote hasa kwenye miradi ya kimkakati tunatakiwa kuwa nao kuanzia hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi ili kutambua nini wanakifanya na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhakikisha wanaenda sambamba na Sheria ya Mazingira. Mradi wa bomba la mafuta ni mradi mmojawapo ya kimkakati katika nchi yetu utakaoleta tija na faida kwa nchi ”
Pia Dkt. Gwamaka amewapongeza viongozi wa mradi wa EACOP kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kushirikiana na jamii inayozunguka mradi ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia na kuwashirikisha katika kila hatua kadri mradi unavyoendelea kutekelezwa.
Afisa Mazingira kutoka NEMC Bi. Dalia Charles ametoa rai kwa wananchi wa Chongoleani na nchi kwa ujumla kuwa Baraza limejiridhisha na mikakati mahsusi iliyowekwa na wawekezaji kudhibiti mwanya wowote wa athari inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi, hivyo basi mradi huo hautakuwa na madhara na una manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha Diwani wa kata ya Chongoleani Bw. Mwaveso Kassimu Mbega ameuhakikishia umma kua mradi huo umepokelewa vizuri na wananchi wa Kata hiyo ambao wameridhika kuachia maeneo yao ili mradi ujengwe na kuishukuru Serikali kupeleka mradi katika eneo hilo, lakini pia amewaomba wananchi wa Chongoleani kuwa na imani na mradi huo kwani Serikali ina nia njema na wananchi wake haiwezi kupeleka mradi wenye madhara, mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na kwa serikali kwa ujumla.
Naye Mtendaji wa Kata ya Chongoleani Bw. Mohamedi Omari Salimu amesema kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka mradi huo. Wananchi wamepata stahiki zao ikiwa na kulipwa fidia na kumekua na taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya mradi huo