Mtendaji Mkuu wa TOAM, Bakari Mongo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu, haja ya uwepo wa mifumo salama ya uzalishaji chakula nchini.
Mshawishaji wa Kilimo Hai, Paul Chilewa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu, haja ya uwepo wa mifumo salama ya uzalishaji chakula nchini.
Mtaribu wa TABIO, Abdallah Mkindi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu, haja ya uwepo wa mifumo salama ya uzalishaji chakula nchini.
Viongozi wa Kilimo Hai wakiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
………………………………………………..
Na Selemani Msuya
WADAU wa kilimo hai nchini wamesema sera na mikakati mizuri katika sekta ya kilimo itakawezesha mifumo salama wa uzalishaji wa chakula kitakachoweza kutumika katika soko la ndani na nje kwa afya ya mlaji.
Wadau hao kutoka Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO).
Akizungumzia njia hizo, Mtendaji Mkuu wa TOAM, Bakari Mongo, alisema njia za kufanikisha mifumo kuzalisha chakula salama, itafanikiwa iwapo sera na mikakati inayotekelezeka itaandaliwa.
Mongo alisema TOAM kwa kushirikiana Shirika la Alliance for Food Sovereignty in Afrika (AFSA), walifanya utafiti katika nchi 24 za Afrika na kubaini kuwa mifumo ya uzalishaji chakula ina changamoto nyingi hasa katika sera na miongozo.
Alitaja baadhi ya changamoto ambazo wamebaini katika utafiti huo kuwa zinaathiri kwenye mfumo wa uzalishaji chakula ni pamoja na uwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi, joto, mvua hazinyeshi kwa wakati, uharibifu wa mazingira na aina ya pembejeo za kilimo.
Mongo alisema katika kukabiliana na hali hiyo dunia inasisitiza jamii kujikita katika kilimo hai ambacho kimeonekana ni salama kwa mlaji, kiafya na kibiashara.
“Sera zetu zinahimiza matumizi ya mbolea za viwandani, hazihamsishi matumizi ya mboji au samadi, lakini pia hata utunzaji wa mazao hauzingatii mifumo salama wa uzalishaji wa chakula salama kwa mlaji. Tunahitaji Sera zetu zishabihiane, zisikinzane na elimu ya kutosha kwa wakulima na wataalam,” alisema.
Alisema pia wanashauri Serikali kuongeza kasi katika kuandaa mkakakati wa kilimo hai ambao utaweza kutoa muongozo sahihi kwenye eneo hilo ili kufanikisha mifumo ya kuzalisha chakula nchini.
Kwa upande wake Mshawishaji wa Kilimo Hai, Paul Chilewa alisema wanachokifanya ni kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), ambayo hayataki mtu kuachwa nyuma.
Chilewa alisema kwa hali ilivyo sasa kwenye mifumo ya chakula inaonekana watu wengi wameachwa nyuma, akitolea mfano Tanzania ambapo wazalishaji wadogo pamoja na kuzalisha kwa wingi hawajaunganishwa na masoko na mfumo mzima.
“Mfumo wa uzalishaji chakula unapaswa kugusa makundi yote na kuachana na mifumo ambayo inaonekana inaadhari, hili litafanikiwa kwa kuwepo sera nzuri. Hakuna sababu ya uzalishaji kuwa mkubwa huku afya ikitetereka,” alisema.
Alisema wakulima wengi hasa wadogo wanatumia mbegu asili, ila hakuna msukumo mkubwa kutoka kwa mamlaka kuhamasisha kilimo ambacho kinazingatia mifumo salama ya uzalishaji chakula.
“Kwa sasa mbogamboga zinatokana na mbegu, zile za asili hazipo, tunapaswa kubadilika kwa kurejea kwenye mifumo endelevu ya uzalishaji chakula, ile afya kwa jamii na iwe na tija kwa mkulima,” alisisitiza.
Mtaribu wa TABIO, Abdallah Mkindi alisema, ufanikishaji wa mifumo sahihi ya uzalishaji itazingatia uwepo wa sera ya Afrika na kinchi ambayo itaonesha mwelekeo katika eneo hilo.
Mkindi alisema Sera ya Chakula na Lishe inapaswa kufanyiwa maboresho ili ibebe dhana ya mfumo salama wa uzalishaji wa chakula ili kulinda afya za wananchi.
“Kama mnakumbuka zamani watu wenye magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na mengine ambayo yanaathiri jamii yalikuwa yanakuta watu wenye uwezo ila sasa kila mtu anaumwa,” alisema.
Mratibu huyo alishauri nguvu kubwa kwa sasa ielekezwe katika uzalishaji wa mazao kwa njia ya kilimo hai, ambayo imeonesha ni salama na ina uhakika wa soko,” alisema.