***********************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
MUFTI wa Tanzania, Sheikhe Abubakar Zuberi Bin Ali Mbwana, amemteua Abdulwalid Juma kuwa Kaimu Sheikhe wa Wilaya ya Ilemela akichukua nafasi ya Sheikh Hussein Mwamba aliyejiuzulu wadhifa huo.
Akizungumza jana baada ya kumpokea kaimu sheikhe huyo mteule wa Wilaya ya Ilemela, Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza , Alhaji Hasani Kabeke,alisema wameyapokea mabadiliko kutokana na utashi wa kiongozi aliyekuwepo kwa kuzingatia matakwa ya Quran na Katiba ya BAKWATA.
“BAKWATA ni chombo kilichokamilika,kinafuata Quran,Suna na Katiba yake na kwa mujibu wa katiba kuna uongozi wa aina mbili, wa kuchaguliwa na kuteuliwa kama ilivyofanyika kwa kaimu Sheikhe wa Wilaya ya Ilemela,”alifafanua Sheikhe Kabeke.
Alisema kuna mambo mengine yakitokea yanaweza kuleta mabadiliko na mabadiliko yakitokea ni kwa utashi wa mwenye kuteua,mengine ni utashi wa mtu binafsi (kuomba mwenyewe kupumzika), Mwenyezi Mungu (kifo) au Mkutano Mkuu wa BAKWATA.
“Sheikhe wetu aliyekuwepo ameomba kumpumzika na Mufti amemwandikia barua ya kumkubalia na tayari ametuteulia Sheikhe Abdulwalid Juma kukaimu nafasi hiyo ya Wilaya ya Ilemela,kwa mujibu wa Katiba Mutfi akishateua,mkutano mkuu wa wilaya au mkoa haujadili bali unapokea,”alifafanua Sheikhe Kabeke.
Alisema kwa upande wake anampokea na kumshukuru Sheikhe aliyepita (Hussein Mwamba),kajipima na kuona apumzike na Mwenyezi Mungu amlipe kheri kwa mazuri aliyofanya na ataendelea kushirikiana naye.
“Nimempokea kaimu sheikhe (Abdulwalid Juma) kwa dhati ya moya wangu naadhi kumpa ushirikiano kama nilivyopmpa mtangulizi wake na niseme wazi kama aliomba Mufti tuendele kushirikiana na Sheikhe Mwamba,”alisema Sheikhe Kabeke.
Aidha alisema juhudi na safari ya kuyaendea maendeleo ni ngumu,inahitaji uvumilivu na subira hivyo ni imani yake kuwa BAKWATA Mwanza inataka kutoka kwenye maneno kwenda kwenye vitendo.
“Safari ya aina hii ni ngumu kidogo, tunapita kwenye miiba mikali,sasa safari hiyo si nyepesi inahitaji uvumilivu,subira na weledi lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutafika,lengo ni kuhakikisha tunakwenda kujenga vituo vya afya kila wilaya,” alisema Sheikhe Kabeke.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza aliahidi ushirikino wa dhati kwa sheikhe huyo mteule lengo afahamu safari yao anayotaka Mufti Zuberi ni kuona wanaibadilisha BAKWATA na taswira ya Uislamu nchini na wao viongozi wa mikoa walioaminiwa wanaona vyema wamuunge mkono Mufti kuyafikia maono aliyonayo.
Kwa upande wake sheikhe Juma,alisema amepokea uteuzi huo wa Mufti wa Tanzania kwa moyo mkunjufu, kwamba hakutuma maombi isipokuwa kwa hekima za Mufti Zuberi na wasidizi wake baada ya Sheikhe Mwamba kuomba kupumzika waliona wamteue kushika nafasi kuwa ana uwezo wa kuitendea haki.
Kaimu sheikhe huyo wa Wilaya ya Ilemela aliahidi kutowaangusha katika wadhifa huo mpya,atatumia nguvu zake na akili aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu wakati wakisubiri uchaguzi wa Mwenyekiti wa Wilaya hiyo.