Na Dotto Mwaibale, Singida
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida Singida limefanya misako mbalimbali yenye kulenga kuimarisha ulinzi na usalama ambapo katika misako hiyo limeweza kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na wizi wa vitu mbalimbali.
Misako hiyo ilifanywa na jeshi hilo kuanzia Novemba 18/2021 hadi Desemba 14,2021.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa alisema kuwakamata mahalifu hao ni mafanikio makubwa kwa jeshi hilo.
Mutahibirwa akizungumzia dawa za kulevya alisema katika kipindi hicho wamefanikiwa kukamata madawa aina ya bhangi misokoto 667 na mbegu za bhangi kg. 1 ambapo walikamatwa watuhumiwa watatu, akiwemo mtuhumiwa wa kiume anayetambulika kwa jina la Manjoli Manjoli (52) Mkazi wa Mtaa wa Utemini Singida ambaye alikamatwa akiwa na misokoto 550 ya bhangi na kuwa watuhumiwa hao ni wauzaji na watumiaji wa bhangi.
Alisema katika msako huo pia yalikamatwa madawa ya kulevya aina ya mirungi rumbesa 48 sawa na kg.26 pamoja na watuhumiwa wawili wanawake waliokuwa wakiyasafirisha wakitokea mkoani Mwanza kuja Singida.
Aidha Kamanda Mutahibirwa alisema katika msako huo walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wa wizi wa pikipiki ambao kesi zao zilishafikishwa mahakamani ambapo vitu vingine vilivyopatikana ni video pc 2 na Radio aina ya subwoofer 2.
Alisema mafanikio hayo yametokana na taarifa za kiintelijensia zinazotolewa na raia wema wanaopenda Mkoa wa Singida uendelee kuwa salama ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Singida kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu zitakazosaidia kuwabaini watu wanaopanga kufanya uhalifu ili uhalifu huo uzuiwe au watuhumiwa wakamatwe mapema kabla ya kuleta madhara.
“Wananchi wanatakiwa kuachana kabisa na biashara haramu zikiwemo biashara za dawa za kulevya aina mbalimbali badala yake wafanye kazi halali ambazo ziotawapatia kipato” alisema Mutahibirwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawaomba wananchi wote waliopotelewa au kuibiwa vitu kufika katika Kituo cha Polisi Singida wakiwa na risiti halali za manunuzi ya vitu hivo ili kuweza kutambua mali zilizokamatwa.