…………………………………………………
Dar es salaam:
Kampuni ya teknolojia na mawasiliano nchini, Vodacom Tanzania PLC leo imetangaza kuwa itatoa jumla ya TZS 4.9 bilioni kama gawio kwa wateja wake wa M-Pesa ambao wametumia huduma hiyo robo ya tatu ya mwaka huu (Julai hadi Septemba).
Akiongea juu ya hili, Mkurugenzi wa M-Pesa Bwana Epimack Mbeteni alisema kuwa faida italipwa kwa wateja wote, mawakala wa rejareja na washirika wengine wa biashara wa M-Pesa ambao watapokea malipo kutokana na huduma ya malipo waliyofanya kupitia simu zao za mkononi.
“Huduma yetu ya pesa kupitia simu za mkononi, M-Pesa, inaendelea kuwa hadithi ya mafanikio ya kushangaza, ikitoa thamani kubwa ya kijamii na kifedha kwa Watanzania. Tumeona ukuaji mkubwa kwenye jukwaa la M-Pesa na wateja zaidi, mawakala, wafanyabiashara na taasisi zinazofanya biashara kufikia karibu TZS bilioni 100 kila siku. Leo tunayo furaha kushiriki katika utoaji wa gawio la Shilingi 4.9 bilioni kwa wateja wetu zaidi ya milioni 8 kote nchini, ”alisema.
Vodacom Tanzania PLC ina zaidi ya wateja milioni 11 kwenye jukwaa lake la M-Pesa inayomiliki sehemu ya soko ya asilimia 40 kulingana na takwimu za TCRA za hivi karibuni. Hadi sasa kampuni imelipa jumla ya Tsh bilioni 167.8 ikiwa ni riba iliyolipwa tangu Julai 2015 wakati BOT ilipotunga kanuni hiyo.
Mbeteni ameongeza kuwa sehemu ya faida kwa kila mteja imehesabiwa kulingana na namna mteja alivyotumia huduma ya M-Pesa pamoja na mambo mengine, kiwango cha shughuli ambazo wamezifanya kupitia M-Pesa kwa kipindi hicho.
“Tumeanza kusambaza pesa kwenye akaunti za wateja wa M-Pesa. Wateja wanaweza kutuma neno KIASI au AMOUNT kwenda 15300 kwa ujumbe mfupi ili kujua ni kiasi gani cha faida watakachopokea. Baada ya kupokea kiasi kilichotolewa, wateja wa M-Pesa wanaweza kutumia pesa hizo kulipia huduma au kufanya matumizi ya aina yeyote wanayojisikia,”aliongeza.
“Tutaendelea kuongoza katika ubunifu, kuleta Watanzania wengi katika uchumi jumuishi wa kidijitali, kuongeza idadi ya wateja wanaotumia huduma ya M-Pesa kupitia simu za mkononi na kupanua huduma zetu za biashara, tukizingatia ushirikiano wa kimkakati na kudumisha aina anuwai za huduma ambazo hufanya malipo haraka, rahisi na salama kwa wafanyabiashara na watu binafsi vile vile,” Mbeteni alihitimisha.
Kuhusu Vodacom M-Pesa Tanzania
Vodacom M-Pesa ni huduma ya kifedha kwa njia ya simu inayoongoza nchini iliyoanzishwa na Vodacom Tanzania PLC mwaka 2008. Kwa sasa ni moja ya huduma chache duniani zilizopewa tuzo ya ubora ya GSMA na ina wateja zaidi ya milioni 10. Kwa kiasi kikubwa M-Pesa imechangia katika kukua kwa huduma za kifedha na shughuli za uchumi nchini. Wateja wanatuma na kuweka pesa kupitia huduma ya M-Pesa kupitia kwa mawakala zaidi ya 106,000 nchini kote. Mfumo wa M-Pesa unaunganisha mabenki, makampuni na mashirika ya Serikali katika kufanya malipo ya kidigitali.