Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,dokta Athumani Kihamia akizungumza katika kikao hicho
Mwakilishi wa Katibu mkuu wa wizara ya mifugo na uvuvi ,Dokta Asimwe Lovince akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha
Wadau wa kikao cha mapitio ya sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006 wakiwa katika kikao hicho jijini Arusha (Happy Lazaro)
………………………………………………………..
Happy Lazaro,Arusha
Wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma ,sekta binafsi na asasi za kiraia wamekutana jijini Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho jijini Arusha ,Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha,Dokta Athumani Kihamia amesema kuwa,sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006 imekuwa ikitekelezwa na wadau mbalimbali ambapo kwa takribani miaka 15 tangu kuanza kutekelezwa kwa sera mafanikio mbalimbali yamepatikana.
Alisema kuwa,mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la Taifa kutoka wastani wa Trilioni 1 mwaka 2006/07 na kufikia wastani wa shilingi Trilioni 10.6 mwaka 2020/21 ,ambapo kwa mujibu wa Takwimu kutoka ofisi ya Takwimu ya Taifa kwa mwaka 2021 ,pato la Taifa ni 148.5 Trillioni.
Dokta Kihamia alisema kuwa, Kati ya mwaka 2006/07 na 2020/21 idadi ya mifugo imeongezeka kutoka ng’ombe milioni 18.5 hadi milioni 33.9 ,mbuzi kutoka milioni 13.1 hadi milioni 24.5 ,kondoo kutoka milioni 3.5 hadi milioni 8.5 ,huku kuku milioni 30 hadi milioni 87.7.
“Kumekuwepo kwa ongezeko la idadi ya viwanda vya kusindika maziwa kutoka viwanda 22 mwaka 2005/06 hadi viwanda 105 mwaka 2020/21 huku kwa upande wa kaskazini tunajivunia kuwa na viwanda vikubwa vya kusindika mazao ya mifugo vikiwemo vya kusindika maziwa vya Tanga fresh na Kilimanjaro fresh “alisema Dokta Kihamia.
Dokta Kihamia alisema kuwa , mafanikio hayo katika sekta ya mifugo yamechangia kuwainua wananchi kiuchumi,kuchangia upatikanaji wa malighafi katika viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya mifugo na kuwezesha biashara ya mifugo na mazao ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Aidha Kihamia alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo kuwa ni Kasi ndogo ya wafugaji kupokea na kutumia yeknolojia bora za uzalishaji mifugo zinazoendana na wakati ili kuongeza tija ,uhaba wa miundombinu ya ukusanyaji na uhitaji wa maji kwa ajili ya mifugo,sambamba na uwepo wa watoa huduma na pembejeo za mifugo wasiokidhi ubora na viwango vya kitaalamu .
Naye Mwakilishi wa Katibu mkuu wa wizara ya mifugo na uvuvi,Dokta Asimwe Lovince alisema kuwa,kikao hicho kimeshirikisha wadau hao kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,Tanga,na Manyara ili waweze kuchangia mawazo yao na uzoefu katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006.
Alisema kuwa,serikali imeweka utaratibu wa kuwa na sera ili kutoa mwongozo wa maeneo ya kufanyiwa kazi kwa pamoja Kati ya serikali na sekta binafsi na hivyo kufikia malengo yaliyotarajiwa kwa maendeleo ya sekta husika.
“kupitia kikao hiki na vikao vingine vya kikanda vitakavyofanyika mwakani mwezi januari na febuari,wadau wa sekta ya mifugo watapata nafasi ya kutoa uzoefu wao katika utekelezaji wa sera iliyopo,na kuainisha changamoto za kisera wanazokutana nazo kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza Kati ya mwaka 2006 na 2021 ili waone uwezekano wa kutatua changamoto hizo kupitia marekebisho ya sera.”alisema .
Aliongeza kuwa, katika kufanikisha mapitio ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2006,shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO) limeonyesha nia ya kushirikiana na wizara kwa kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu ili kufanikisha zoezi hilo.