Leo tarehe 12 Desemba 2021 Muwakilishi wa Kampuni ya Southwest Exporters kutoka Texas Marekani inayojishughulisha na bidhaa za mazao ya misitu kama vile fanicha, malighafi za kutengeneza boti Bw. Vinod Nair ametembelea banda la Tanzania kwenye maonyesho Expo 2020 Dubai.
Amekutana na kufanya mazungumzo na muwakilishi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – Tanzania Forest Services Agency (TFS) katika maonyesho ya Expo 2020 Dubai Bi. Martha Chassama.
Bw. Nair ameeleza nia ya kuvutiwa na biashara ya mbao zinazotokana na miti ya misaji ambapo alihitaiji kufahamu zaidi ni maeneo yapi ambayo yanasimamiwa na TFS na yanatumika kwa ajili ya uzalishaji wa miti ya Misaji.
Bi. Chassama amemueleza Bw.Nair kuhusu upatikanaji wa miti ya misaji, taratibu za ulipaji wa tozo na ada mbalimbali, muda unaotumika kusafirisha malighafi za miti ya misaji kutoka Tanzania hadi kufika katika nchi husika na taratibu nyingine muhimu.
Ameongeza kuwa uzalishaji wa Miti ya misaji huchukua takribani miaka 20 kufikia kiwango cha ubora kinachofaa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za mbao zenye kiwango.
Moja kati ya masuala muhimi ambayo muwekezaji anapaswa kufahamu kabla ya kuja kuwekeza kwenye Sekta ya Misitu na Nyuki ni upatikanaji wa usajili wa biashara ya mazao ya misitu na leseni ya uvunaji, usafirishaji wa mazao ya Misitu na Nyuki, taratibu za usafirishaji bandarini na nchi kavu na taratibu zote za ukaguzi.
Aidha, katika mazungumzo hayo Bi. Chassama amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau na uwekezaji wenye nia ya kufanya biashara na Tanzania hususani upande wa bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu na nyuki na kuwekeza kwenye utalii Ikolojia. Amesema,” Tanzania imejipanga katika kupokea wawekezaji na tunategemea waje kwa wingi ili kwa pamoja tutumie fursa hii ya uwekezaji kuleta maendeleo yenye tija ya pamoja kati yao na Taifa kwa ujumla”.
Vilevile alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine wa aina hii kuja kuwekeza katika utalii wa ikolojia ikiwa ni moja kati ya vipaumbele vinavyoitangaza Tanzania Ulimweguni kwenye maonyesho ya Dunia ya Expo 2020 Dubai.
Maonyesho haya yalianza tarehe 01 Oktoba 2021 yakizileta pamoja nchi 192 ulimwenguni na yanatajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Machi 2022.