ADELADIUS MAKWEGA,DODOMA
Wakaazi wa vijiji vya Mkelezange,Mkamba, na Kimanzicha miaka 1980 walikuwa pia ni wakulima wa zao la Korosho ambalo lenyewe lilikuwa zao la msimu zilikuwa zikinunuliwa na kuhifadhiwa katika maghala maalumu na kuna wakati malori makubwa yalikuja na kuzisomba na kuondoka nazo.
Thamani ya Korosho kwa wakati huo japokuwa nilikuwa mdogo niliitambua kwa kuwa watoto wadogo wengi wakati huo walikuwa na mchezo unaitwa Kisago(sago). Mchezo huu ni kama kamali ya korosho. Ambapo kabla ya kuanza, anapita kijana mmoja majumbani akinadi na kuwajulisha wenzake kuwa sasa ni wakati wa kucheza kisago.
“Kisago, Kisago, Kisago, Kisago, Juma Kisago, Hamisi Kisago, Mohammed Kisago, Abdalla Kisago, John Kisago, Muhsini Kisago.”
Huku akiwa na mfukoni amejaza korosho zake na betri chakavu mkononi kama nyenzo ya kuchezea mchezo huo. Wakati mwingine huwa wanatumia vigae vya vyungu vilivyovunjika badala ya betri.
Baada ya watoto kunadiwa hivyo hutoka majumbani mwao na kukusanyika pamoja na kukubaliana kama watacheza kwa kutumia betri la zamani au vigae, hapo wataangalia je kila motto/mchezaji analo betri? Kama wakigundua yupo ambaye hana, basi maamuzi ya pamoja yanafanywa ili kutumia vigae, maana kila nyumba huwa na vigae vya vyungu vilivyovunjika.
Baadaye linachorwa dimba la duara alafu wanakubaliana kuwa kila mchezaji ataweka korosho ngapi, kati ya 5-20 na kama kuna wachezaji kumi, dimba linakuwa na korosho 200, hizo huwa zadi ya kilo 2 za korosho. Maana kilo moja ya korosho inaweza kuwa na korosho kati ya 50-60 kulingana na ubora wake.
Mchezaji mmoja anaweza akahesabu umbali baina ya dimba na wanapotupia betri/vigae Hapo watajipanga mstari kama watoto wanaoshindana riadha alafu wanakubaliana kuanza kurusha betri kuelekea dimbani kwa majina au vyovyote watakavyokubaliana, mchezo huo kuanza.
Baadaye wachezaji wote watakuwa jirani na dimba na kuzilenga na kuzitoa korosho dimbani hadi mshindi akipatikana, pale ukikosa unampisha mwenzako na anaendelea.
Pia wanaweza kucheza kwa namna nyingine kwa mtoano wanarusha betri bila dimba alafu kila mmoja anaanza kutafuta kuigonga betri la mwenzake na yule anayegongwa anamlipa kiasi kadhaa cha korosho mwenzake kulingana na makubaliano yao.
Baada ya kucheza mchezo huo mtoto aliyeshinda anaweza akawa na hata kilo 5-10 za Korosho na mara nyingi mchezo huo ulikuwa unachezwa wakati wa likizo za shule mwezi wa 12 na ndipo korosho huwa zinavunwa sana.
Watoto walikuwa wanaenda kuokota korosho hata kwa ujanja ujanja kwenye mashamba ya watu ili mradi akacheze KISAGO. Kwenda huko katika mashamba ya watu ilikuwa mwiko kwani kuna mashamba ukifika katika miti unakutana na karatsi zilizokuwa zimeandikwa maandishi ya kiarabu kwa rangi nyekundu .
Mashamba mengine unakutana maandishi ya kiarabu yameandikwa katika vifuu vya nazi katika kila mpaka. Hapo watoto wengi walikuwa waoga kusogelea shamba hilo kuopa kuvimba matumbo au kufa, maana mwenye shamba hapo huwa ametega mtego kwa wezi..
Wakishacheza Kisago watoto marafiki wanaweza kuzikaanga na kula au kuzikaanga na kuziuza barazani nyumbani na wakati mwingine kuwapelekea wale wanaonunua korosho zisizobanguliwa. Kwa hakika mchezo huu ulikuwa ukimjenga mtoto aliyezaliwa katika eneo linalozalisha korosho kutambua thamani yake. Kwanza kujua umuhimu wa kuwa na mikorosho yake mwenyewe na pili kwa kutambua thamani yake wakati wa kuuza.
0717649257