Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi
Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Yusuph Singo akiteta jambo na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi wakati wa uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2022. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Executive Solutions, Aggrey Marealle ambaye kampuni yake inaratibu mbio hizo kitaifa.
************************
Mdhamini mkuu wa mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon, Kilimanjaro Premium Lager ameahidi mbio kubwa zaidi yenye matukio ya kusisimua wakati mbio hizo zinatimiza miaka 20 tangu kuanishwa kwake.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, alisema huku ikiwa imebaki miezi miwili na nusu kabla ya kufanyika kwa mbio hizo, wao kama wadhamini wakuu wanashirikiana kwa karibu na waandaaji kuhakikisha shughuli hiyo ya miaka 20 inafana kabisa.
“Mashindano yajayo ya Kilimanjaro Marathon yatakuwa ya hatua muhimu haswa ikitiliwa maanani ya kuwa chapa ya Kilimanjaro Premium Lager imekuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita.
“Tunatarajia kuyafanya mashindano hayo ya maadhimisho ya miaka 20 kwa namna ya pekee, kwani ni ya kihistoria kutokana na ukweli ni moja ya udhamini mrefu kupitia chapa ya Kilimanjaro Premium Lager na ambayo imeifanya chapa hiyo kukua mwaka hadi mwaka”, alisema na kuongeza, tumeguswa pia na umuhimu wa mashindano haya kukuza utamaduni wa Mtanzania pamoja na utalii kwa ujumla.
“Tumetenga zawadi za kifedha zenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 22, ambapo washindi wa kwanza katika mbio za 42km, kwa wanawake na wanaume watapata zawadi ya shilingi milioni 4 za Tanzania kila mmoja”, alisema na kuongeza katika mbio hizo za kilometa 42 kutakuwa na motisha ya ziada ya shilingi milioni 1.5 kwa kila Mtanzania atakayemaliza wa kwanza upande wa wanaume na wanawake” alisema.
Alitoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema wakati zoezi hilo litakapoanza rasmi Oktoba 17, 2021, kupitia anuani ya mtandano www.kilimanjaromarathon.com na kupitia Tigo Pesa kwa kupiga * 149 * 20 #. “Nitoe wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizi kuchangamkia fursa ya punguzo la asilimia 20 kwa wale watakaojiandikisha kuanzia Oktoba 17, 2021 hadi Januari 7, 2022, baada ya hapo watakaojiandikisha watalipa malipo yaliyowekwa na wandaaji”, alisema.
“Sisi kama TBL tutawakilishwa na baadhi ya wafanyakazi ambao watakimbia mbio tofauti tofauti na tayari wameshaanza mazoezi ili kujiandaa na mbio hizi kubwa Afrika Mashariki na Kati ambazo huleta pamoja washiriki zaidi ya 11,000 kutoka mataifa zaidi ya 55,” alisema.
Wadhamini wa Kilimanjaro Marathon 2022 ni Kilimanjaro Premium Lager-42km, Tigo- 21 km Half Marathon, Grand Malt-5km, wadhamini wa meza za maji ni Absa, Unilever, TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, na wasambazaji maalumu, GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles.
Mbio za mwakani zitafanyika katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi Februari 27, 2022.
Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions Limited.