………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MKUU wa wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani Sara Msafiri ,amepiga marufuku ujenzi katika eneo la Mitamba ambalo ni la Serikali na kusisitiza wavamizi wote wanaokaidi agizo la kuondoka na kuacha kujenga katika eneo hilo wajue WAMEPOTEZAAA.
Akizungumzia wavamizi katika eneo hilo ,amekemea kutumia nguvu kwenye kujenga maeneo ya Serikali ama yenye hati Halali pasipo kufuata taratibu.
“Tusiwekeze nguvu nyingi za kujenga kwenye maeneo ya Serikali,nimepita eneo la Mitamba, nimeona kuna nyumba nzuri zilizogharimu hadi milioni 100, Niwaambieni kufanya hivyo ni kujitafutia umaskini kwa gharama nafuu,”
“Mtu anapojenga lazima ajinyime sana,Wapo akinamama ambao wamejinyima kwa kuvaa kanga moja kwa muda mrefu,kucheza vikoba ili wajenge, Lakini wamejenga kwenye maeneo ya Serikali,HAPO WAMEPOTEZA”alisema Sara.
“Hakuna hata siku moja Serikali itakuja kuwaachia maeneo mlipovamia,hata kama itaacha itatoa kwenye Mamlaka za upangaji yaani Mkurugenzi wa Halmashauri,hapo ni kwamba kama umejenga katika eneo la Serikali ni sawa na mtu anaelala nje “alifafanua Sara.
Mkuu wa wilaya hiyo ya Kibaha , ameeleza ifikie hatua watu wakaheshimu ardhi za Serikali na zinazotambulika kihalali na kuacha tabia ya kuvamia maeneo yasiyo ya haki kwao.
Alitoa rai kwa wavamizi kuondoka na kuacha kujenga eneo la Mitamba ,na anaekaidi ajue anajidanganya kuwa atapata haki ama kulipwa au kuachiwa kirahisi eneo hilo .