Sadock Maningo akiwa na wakili wa kituo sheria na haki za Binaadamu (LHRC) Hamis Mayombo nyumbani kwake anapopinga Nyumba kubomolewa
Diwani wa viti maalun Eliza Malembera
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamichere Timus Chacha
**********************
Na Mwandishi Wetu, TARIME
Mkazi wa Kitongoji cha Kigonga B kilichoko Kijiji cha Matongo, Kata ya Matongo wilayani Tarime, Sadock Maningo amegoma kubomoa nyumba zake ili kupisha upanuzi wa mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mar huku wananchi wengine zaidi ya 1900 wakitaka usaidizi wa kisheria baada ya kusubiri miaka tisa kulipwa fidia.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwame Manongi alisema amekataa kupokea Sh. milioni 62.905 zilizopendekezwa kulipwa kwake kama fidia ya ardhi, mali na usumbufu kwani ni kiasi kidogo hakilingani na thamani ya nyumba na ardhi yake.
“Kama unavyoona hapa kwenye nyaraka, tathmini ya kwanza ilifanyika Septemba 26 mwaka juzi (2019). Wakasema mali zangu zote hapa zina thamani ya Sh. milioni 129 (takwimu halisi zilizopo kwenye nyaraka ni Sh. 129,354,560).
“Nilikubali kulipwa kiasi hiki cha fedha maana walau kilikuwa kinaakisi thamani ya mali zangu, lakini cha kushangaza nilipokwenda Ofisi ya Uhusiano (ya Barrick North Mara) nilikuta malipo yangu ni Sh. milioni 62 (takwimu halisi Sh. 62,905,384.72)”alisema
“Nilishtuka sana, nikakataa kabisa kusaini hizi nyaraka za malipo. Tathmini ya pili ilifanyika Mei 11 mwaka huu (2021). Wamesema eneo langu na vilivyomo thamani yake ni Sh. milioni 83 (takwimu halisi Sh. 83,716,994).
“Nimekataa pia kusaini malipo haya kwa sababu ninaona ninapunjwa. Ninataka wanilipe kulingana na tathmini ya mwanzo kabisa (Sh. milioni 129)”aliongeza.
“Nipo hapa tangu mwaka 1994, eneo hili nilipewa na baba yangu mzazi. Ninatambua kuishi karibu na mgodi wa madini ni hatari lakini siwezi kukubali kuliachia eneo hili (lina ukubwa ekari 1.386) kwa malipo hayo wanayotaka wao. Vifaa vya ujenzi vimepanda bei. Nitawezaje kujenga tena nyumba zote hizi kwa Sh. milioni 83.” Alihoji.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Maningo, kwenye Kitongoji cha Nyamichere, Kijiji cha Nyakunguru, wakazi wake wamesubiri fidia ya kupisha upanuzi wa mgodi huo wa dhahabu kwa miaka tisa sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Timus Chacha, anabainisha kuwa familia 1,900 zimeathiriwa na kuchelewa huko kwa fidia hiyo, akikumbusha kuwa mpaka sasa tayari kumeshafanyika tathmini ya maeneo yao mara tatu.
“Maeneo yote yaliyofanyiwa uhakiki tumezuiwa kufanya shughuli za maeneo. Miaka tisa sasa hatufanyi chochote kwenye maeneo yetu na hatujui hatima ya fidia yetu,” anasema.
Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Ingwe, Eliza Malembera, anasema amefuatilia suala la fidia kwa wananchi wakena kupatiwa mrejesho kwamba uongozi wa mgodi umeamua kuachana na mpango wa kutwaa maeneo hayo, hivyo yatabaki kuwa mali ya wananchi.
“Sasa unajiuliza hawa wananchi wamezuiwa kufanya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao toka mwaka 2012, leo unawaambia huna mpango na maeneo yao tena.
“Tumelifikisha suala hili kwenye vikao vya Baraza la Madiwani lakini bado kimya kimetawala japo alifika mmoja wa maofisa wa mgodi kwenye moja ya vikao vyetu akasema eneo hili hawalihitaji tena.
“Aliahidi kuwa watalipa fidia kidogo ya usumbufu. Waliahidi kuwa ingelipwa Septemba mwaka huu lakini hadi sasa (Novemba 21, 2021) hakuna kilicholipwa kwa wananchi.
“Ukweli ni kwamba wananchi wamepata hasara kubwa kutokana na kusimamishwa kuendeleza maeneo yao kwa kipindi chote hicho cha miaka tisa,” anasema.
Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Ofisi ya Arusha, Wakili Hamisi Mayombo, anasema wanafuatilia kwa karibu yanayoendelea Nyamongo.
Wakili Mayombo anasema kwamba baada ya kufuatilia suala la Maningo, kituo chao kinaona mwananchi huyo anastahili kulipwa Sh. milioni 129.354 ya fidia ya mali zake ili kupisha upanuzi wa mgodi na si vinginevyo.
“Kuhusu wakazi wa Kitongoji cha Nyamichere, LHRC tumeamua kuwasaidia kufungua shauri mahakamani ili kudai haki yao ya fidia.
“Tumeona kuna shida mgodi kuzuia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao halafu baada ya miaka tisa uongozi wa mgodi useme hauna mpango na maeneo hayo. Hii sio sawa, sio haki,” anasema.
Ofisa Uhusiano wa Barrick North Mara, Gilbert Mworia, ambaye anakiri bado hawajamlipa fidia Maningo kutokana na mkazi huyo wa Kijiji cha Matongo kukaa kutia saini nyaraka za malipo zilizoandaliwa.
“Sisi (Barrick North Mara) tuko tayari kumlipa hata leo. Shida ni kwamba kwa sasa tunatumia maofisa wa serikali kufanya tathmini ya maeneo yote tunakohitajika kulipa fidia.
“Sasa nyaraka za kumlipa huyo jamaa (Maningo) tulizopewa zinasema alipwe Sh. milioni 83. Tukimlipa zaidi ya hapo tutaingia kwenye makosa ya utakatishaji.
“Hapo anapoishi ni karibu sana na mgodi, ni hatari kiusalama. Tutakwenda kuzungumza naye tena ili akubali kulipwa fidia aondoke kwenye eneo hilo,” anasema.
Kuhusu wakazi wa Nyamichere, Mworia anasema wameamua kutoyatwaa maeneo yao kwa kuwa mgodi umebadili mpango wa uchimbaji.
“Kwa kuwa maeneo yale yamekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa, wamiliki wake watalipwa kifuta jasho, lakini lazima tufanye uhakiki kwanza maana huku kuna ujanja ujanja mwingi sana linapokuja suala la kulipa fidia,” Mworia anahitimisha.