Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilber Ibuge akipiga lipu katika moja ya madarasa yanayojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid 19 katika shule ya sekondari Muhesi wilaya ya Tunduru jana,anayemuangalia ni Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wa kwanza kulia akimsikiliza mhandisi wa ujenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alipokwenda kukagua ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa vinavyojengwa katika shule hiyo kupitia fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid -19,wa pili kulia mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro na katikati Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza jana na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Muhesi wilaya ya Tunduru alipokwenda katika shule hiyo kwa ajili ya kukagua na kushiriki ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa vinavyojengwa na Serikali kupitia fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19,aliyesimama nyuma ya Mkuu wa mkoa ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro.
…………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Tunduru
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amekagua miradi ya ujenzi wa madarasa inayotekelezwa chini ya mpango wa maendeleo na usatwi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Brigedia Jenerali Ibuge, ameipongeza Halmashauri hiyo kutokana na kujenga madarasa kwa viwango na ubora wa hali ya juu, licha ya kushindwa kukamilisha kwa muda uliopangwa ambao ni tarehe 10 mwezi huu ambapo ameongeza siku tatu hadi tarehe 13 kwa Halmashauri zote za mkoa huo ziwe zimekamilisha ujenzi wa madarasa.
Alisema,baadhi ya Halmashauri za mkoa huo bado hazijakamilisha ujenzi wa miradi hiyo,hivyo amewataka viongozi na watendaji waliopewa dhamana kusimamia kazi hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati uku wakizingatia ubora na thamani ya fedha zilizotolewa na kutumika.
Jenerali Ibuge,amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo,kuhakikisha zinakabidhi kazi hizo zikiwa zimekamilika ifikapo Desemba 14 mwaka huu.
“nawataka wakurugenzi wa Halmashauri chini ya usimamizi wa wakuu wa wilaya kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilike kwa wakati ili kuondoa tatizo la watoto kubanana madarasani na kuwawezesha kupokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani”alisema Ibuge.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema,wilaya hiyo imejipanga kukamilisha miradi ya ujenzi yote ifikapo tarehe 14 mwezi huu, na kueleza kuwa kukamilika kwa madarasa hayo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Mtatiro amemuhakikishia Mkuu wa mkoa kuwa,watashughulikia changamoto na watayafanyia kazi maelekezo yake kuhusiana na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando alisema, Halmashauri imepokea fedha jumla ya Sh.6,185,058,730.14 kati ya hizo Sh.378,981,643.88 zikiwa mapato ya ndani,Sh.5,806,077,086.26 ruzuku ya maendeleo ya Serikali kuu na wahisani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha alisema, wamepokea Sh.2,941,412,138.30 kutoka Shirika la Fedha Duniani(Covid- 19)kwa ajili ya kujenga vyumba 122 vya madarasa,nyumba za watumishi,jengo la dharura,uhamasishaji wa chanjo dhidi ya Covid-19 na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.
Marando amemshukuru Rais Samia Hassan kwa kuipatia Halmashauri hiyo fedha nyingi ambazo zimekwenda kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo elimu,maji,afya,umeme, na barabara.