Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika maandamano ya kitaaluma wakati wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru mkoani Arusha
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na wahitimu, wakufunzi wafanyakazi na wananchi wakati Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru mkoani Arusha.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizindua Programu ya “She Brave why not me?” yenye lengo la kuhamasisha Wanawake kupinga ukatili wa Kijinsia, wakati wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitia Saini katika bango la Programu ya “She Brave why not me?” yenye lengo la kuhamasisha Wanawake kupinga ukatili wa Kijinsia, wakati wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akimtunuku Shahada ya Uzamili Ahadi Faustin mmoja wa wahitimu wa Shahada ya Maendeleo
Baadhi ya Wahitimu wa Astashahada, Stashahda, Shahada na Shahada za Uzamili kutoka katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru wakifuatilia sherehe za Mahafali ya 11 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika mkoani Arusha.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
…………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum Tengeru Arusha
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameitaka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinavyosimamiwa na Wizara kutambua kuwa njia pekee ya kuwasaidia wahitimu kuweza kupata ajira ni kujiajri na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema leo mkoani Arusha wakati wa Mahafali ya 11 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo jumla ya wanafunzi 1440 wamehitimu katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahadi na Shahada za Uzamili.
Naibu Waziri Mwanaidi amewataka wahitimu kutumia Taaluma kwa kuhakikisha wanasaidia kuamsha Ari ya Jamii kushiriki katika maendeleo kwa kutumia rasimali zinazowazunguka ili kutatua changamoto za kimaendeleo.
“Mkawe mabalozi huko muendako mkahimize wananchi kujitoa katika ujenzi wa miundombinu hasa vituo vya Afya na madarasa katika kusaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Ameongeza kuwa wahitimu wa Mwaka huu wameandika historia kwani ni mwaka ambapo Tanzania Bara inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru hivyo wanatakiwa kuiweka historia hiyo kwa vitendo kwa kuhakikisha wanaleta matokeo chanya katika jamii zao na kuwa wabunifu na kutumia changamoto zilizopo kuwa fursa za kimaendeleo.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi ameiagiza Taasisi hiyo kuendelea kusimamia utoaji wa Taaluma kwa kuzingatia weledi na viwango vilivyowekwa na Mamlaka mbalimbali za elimu ili kutoa wahitimu waliofuzu kwa viwango husika.
Awali akitoa taarifa ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Bakari George amesema kuwa Taasisi inaendelea kuhakikisha inatoa Taaluma kwa kuhakikisha wakufunzi wanaongeza ujuzi zaidi ili kuboresha taaluma inayotolewa katika Taasisi hiyo.
Ameongeza kuwa Taasisi imefanya mapito ya maboresho ya Mpango wa Taasisi hiyo na kuongeza Kituo cha Ubunifu cha Kidijitali na Maktaba ya Nyaraka za Wanawake ili kuhakikisha inashirikiana na jamii inayowazunguka na kutatua changamoto zilizopo katika jamii husika.
“Katika hili tunahakikisha wanafunzi wanafanya kazi kwa vitendo kwa kushirikiana na jamii inayotuzunguka ili kuwapa ujuzi wa namna watakavyokabiliana na kusaidia kutatua changamoto za kimaendeleo wanaporudi katika jamii zao” alisema Dkt Bakari.
Aidha amesema kuwa kwa mwaka fedha 2019/2020 Taasisi ilipata fedha jumla ya Shillingi Billioni 2.6 ambazo zinatumika katika ujenzi wa kumbi pacha za mihadhara na bweni kwaajili ya wanafunzi wa kike ambayo kwa ujumla yamefikia asilimia 50 ya ujenzi wake.
“Mhe. Mgeni Rasmi naomba utufikishie Asante na salamu zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuwezesha kupata fesha za maendeleo ambazo zinasaidia kutatua changamoto zinazoikabili Taasisi yetu” alisema Dkt Bakari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Undeshaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Rosemarie Mwaipopo ameeleza kuwa Bodi anayoiongoza itahakikisha inaisimamia Taasisi na kuhakikisha inakuwa Taasisi ya mfano katika utoaji wa Taaluma hasa ya Maendeleo ya Jamii iyakayosadia kuchagiza Kasi ya maendeleo.
“Napenda kuishukuru Wizara kwa ushirikiano unaotupa katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kuisimamia Taasisi na kuhakikisha inafanya kazi kwa weledi na ubunifu” alisema Dkt Rosemarie
Ameongeza kuwa katika kuiendeleza Taasisi hiyo imejipanga kujenga jengo la Utawala, Kituo cha Kitaifa cha Kidigitali na kuiomba Serikali kuiwezesha Taasisi kupata fedha za maendeleo ili kutekeleza miradi hiyo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa kumbi pacha za mihadhara na bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike ambapo ameiagiza Taasisi kusimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati ili kutatua changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo.
Nao baadhi ya Wahitimu wamesema wanaenda kwenye jamii kufanya kwa vitendo vile ambavyo wamejifunza Chuoni hapo kwa namna ambayo itasaidia kuamsha Ari ya Jamii katika kujiletea maendeleo.