Mkutano wa 21 wa Baraza la
Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika
tarehe 10 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa
na mikutano miwili ya awali iliyofanyika tarehe 6 hadi 8 Desemba 2021na tarehe
9 Desemba 2021 katika ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu mtawalia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mkutano huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb) aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo mjini
Zanzibar na kupongeza maamuzi yaliyofikiwa na sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya kwamba mkutano
huo ufanyike mjini humo ili kuwapa fursa wajumbewa mkuano huo kuyafahamu maeneo ya utalii ndani ya kanda.
Vilevile alieleza Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania itaendelea kufanyia kazi maamuzi na mapendekezo mbalimbali yanayotolewa
na vikao hivyo ili yaweze kuwa na tija kwa masalahi ya wananchi ndani ya jumuiya.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta ya Uzalishaji na Jamii, Mhe.
Christophe Bazivamo katika ufunguzi wa
mkutano huo aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapokezi mazuri kwa
wajumbe wa mkutano huo na kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa
Tanzania Bara.
Aidha, alitumia nafasi hiyo
kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki
katika kurasimisha lugha nyingine zitakazotumiwa katika mikutano ya jumuiya
hiyo ambapo, alieleza mpaka sasa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo inafanyia kazi taratibu
za kuifanya lugha za Kiswahili na kifaransa kuwa lugha rasmi kwa ajili ya matumizi ya
mikutano ya jumuiya.
Pia akapongeza juhudi
zilizooneshwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
kwa kuifanya tarehe 7 Julai kuwa siku ya Kiswahili.
“UNESCO imeonesha ni namna
gani lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha pekee ya kiafrika yenye watumiaji
wengi imeweza kuthaminiwa ulimwenguni, sisi kama jumuiya tutaendeleza jitihada
za kukuza Kiswahili” alisema Mhe. Bazivamo.
Kadhalika, Mhe. Bazivamo
amezisisitiza Nchi wanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha zoezi la uandaaji wa
Hati za Kusafiria za Kielekronik za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC e-Passport)
ambapo, ameeleza mpaka sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ndio
imefanikiwa kukamilisha zoezi la ugawaji wa Hati hizo za kusafiria kwa wananchi
wake.
Ujumbe wa Tanzania katika
mkutano huo umeongozwa na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (Mb.) Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ambaye ameambatana na Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri, Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bara.
Viongozi wengine walioshirikia mkutano huo
ni pamoja na; Dkt. Fatma H. Mrisho, Katibu Mkuu Wizara
ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar; Dkt. Othman Mohamed Ahmed, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia – Tanzania Bara, Bw. Eliabi Chodota, Mkurugenzi Idara ya
Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki; na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu
wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Pamoja na
mambo mengine Mkutano
wa 21wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la
Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokea
taarifa ya utekelezaj wa maamuzi/maagizo ya
mikutano iliyopita; hali ya mlipuko wa janga la
UVIKO -19 Kikanda; na Utekezaji
wa programu
na miradi ya Afya.
Ujumbe wa Tanzania |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
Ujumbe kutoka Burundi |
Ujumbe kutoka Uganda |
Picha ya pamoja viongozi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo walioshiriki mkutano. |
Mkutano ukiendelea |