Naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Tulia Ackson akizungumza katika mahafali ya 23 ya chuo Cha uhasibu Arusha (Happy Lazaro)
Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha,Profesa Eliamani Sedoyeka akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha (Happy Lazaro)
Baadhi ya Wahitimu katika Chuo cha Uhasibu Arusha wakiwa katika mahafali yao .
*************************
Happy Lazaro,Arusha
Arusha.NAIBU Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dokta Tulia Ackson amewataka wahitimu kujikita zaidi katika kusomea maswala ya utafiti kwani sekta hiyo ina mchango mkubwa Sana katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika mahafali ya 23 ya wahitimu 2,481 katika chuo cha uhasibu Arusha (IAA) waliohitimu ngazi ya Astashahada, stashahada na shahada ya uzamili yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa AICC.
Amesema kuwa,kama Taifa hivi sasa wanahitaji wasomi waliobobea kwenye utafiti ili nchi iweze kufikia malengo yake kwani bila kuwepo kwa tafiti katika kila eneo hatuwezi kufikia malengo yaliyowekwa.
Tulia amesema kuwa,bila kuwa na wasomi wa kutosha waliobobea kwenye tafiti inakuwa ngumu kufikia malengo sambamba na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii,hivyo amewataka wahitimu hao kujiendeleza zaidi katika maswala ya tafiti kwani ni sekta nyeti na yenye mchango mkubwa kwa Taifa.
Aidha amewataka wahitimu hao kwenda kuunga mkono juhudi za serikali katika maeneo mbalimbali huku akiwataka elimu hiyo kuwa sehemu ya historia ya maisha kwa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wenzao katika jamii inayowazunguka.
“Nawaombeni sana mkafanye jambo la tofauti kwenye jamii ili jamii itambue mchango wenu kwa maendeleo ya nchi na asiwepo hata mmoja miongoni mwenu atakayerudisha nyuma juhudi za serikali bali muwe mabalozi wazuri popote mtakapokuwa.”amesema Tulia.
Naye Mkuu wa chuo hicho,Profesa Eliamani Sedoyeka amesema kuwa,chuo hicho kinatoa mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada,stashahada,shahada na shahada ya uzamili ambapo kuanzia januari mwakani chuo kinatarajia kuanza kutoa shahada ya uzamivu wakishirikiana na chuo Cha Nelson Mandela .
Sedoyeka amesema kuwa,chuo hicho kimejipanga kuwaandaa wataalamu ambao watakidhi vigezo na matakwa ya soko la ajira kitaifa na kimataifa ambapo wanafunzi wanajifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia ambapo wameanzisha pia mfumo wa uanagenzi ambao unawawezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo zaidi katika maeneo ya kazi wakati huo huo wakiwa wanaendelea na masomo.
“Kupitia Kiotamizi na someone la ujasiriamali ambalo linafundishwa kwa wanafunzi wote na kuweza kuandaliwa katika elimu ya darasani,na chuo kimeweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kubuni mawazo ya biashara na kuyafanyia kazi mawazo hayo kuwa biashara halisi,ambapo wanafunzi wote wanasaidiwa na walimu wetu namna ya kuanzisha biashara ndogo ndogo ikiwa ni namna ya kuwajengea msingi wa ujasiriamali ili watakapohitimu wawe na uwezo wa kujiajiri”amesema Profesa Sedoyeka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo Cha uhasibu Arusha,Dokta Mwamini Tulli amesema kuwa,chuo kimeendelea kutoa elimu kwa kutumia mitaala bora inayowaandaa wanafunzi kwa mahiri yenye maarifa yanayohitajika wakati husika.
Dokta Tulli amesema kuwa,wamekuwa wakianzisha kazi mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira la Sasa nchini kwani ni moja ya mikakati ya chuo ,huku chuo kikiendelea kufanya tafiti ili kujua mahitaji ya watanzania na kuweza kuanzisha kozi mbalimbali zinazokidhi mahitaji yao.