Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akigawa chandarua kwa moja ya wazee wa mkoa wa Katavi.
Mwakilishi wa wanawake akipokea chandarua kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Katavi.
…………………………………………………….
Na Zillipa Joseph, Katavi
Wakazi wa mkoa wa Katavi wanaadhimisha miaka sitini ya Uhuru wa Tanganyika kwa kupata vyandarua bure kwa lengo la kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria na hivyo kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda kupitia fursa mbalimbali zilizoko mkoani Katavi.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akizungumza na wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Kashato aliwataka wakazi wa mkoa huo kutumia vizuri fursa walizonazo.
“Sasa hivi mkoa umefunguka, sasa msiache watu wa nje wakaja kutumia fursa hizo” alisema Mrindoko.
Alitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni uwekezaji katika ufunguzi wsa viwanda mbalimbali, kilimo, madini, na utalii.
Aidha kuhusu kujikinga na ugonjwa wa malaria aliwataka wakazi wa mkoa huo kuvitumia vizuri vyandarua hivyo na sio kufugia kuku ama kuvulia samaki.
Awali Mratibu wa Malaria mkoa wa Katavi Ramadhan Karume alisema wametoa vyandarua hivyo ili kuokoa maisha.
Alieleza mafanikio yaliyopatikana kwa miaka kadhaa kupitia matumizi ya vyandarua kuwa yamepunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia hamsini hadi asilimia saba.
‘Tumepita kila mtaa na Kijiji kuhamasisha watu kujiandikisha kuchukua vyandarua” alisema.
Pia aliwasihi wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa matumizi sahihi ili kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukisumbua zaidi kinamama wajawazito na watoto wadogo na wakati mwingine kusababisha vifo