Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa tahadhati kwa Wananchi wa Mkoa huo, kuhusu Makampuni yanayojitokeza kuweka Fedha ili kupata zaidi katika hafla ya ulipaji wa Fedha awamu ya kwanza ,kwa Wahanga waliyoweka Fedha zao katika Kampuni ya Masterlife.
Kamishna wa Bajeti Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Saumu Khatib Haji, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu zoezi linavoendelea la ulipaji wa Fedha kwa Awamu ya kwanza kwa Wahanga waliyoweka Fedha zao, katika Kampuni ya Masterlife, Hafla iliyofanyika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, wakiwa katika zoezi la awamu ya kwanza la kuwalipa Wahanga waliyoweka Fedha zao katika Kampuni ya Masterlife, Hafla iliyofanyika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
PICHA NA MARYAM KIDIKO / MAELEZO ZANZIBAR.
****************************
Na Kijakazi Abdalla Maelezo 8/12/2021
WANANCHI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walioweka fedha zao katika kampuni ya Masterlife wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uwamuzi waliochukua wa kuwalipa fedha zao.
Kauli hiyo waliitoa katika zoezi la utoaji wa fedha hizo lililofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Walisema serikali imechukua uamuzi wa busara kwa kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wapata haki yao.
Walisema awali serikali ilipotangaza kufungwa kwa kampuni hiyo waliingiwa na taharuki na kukata tamaaa lakini baada ya uamuzi huo imeonesha wazi kuwa serikali ipo kwa ajili ya wananchi hasa wenye kipato cha chini.
Nae Miza Khamis Mati mkaazi wa Kigunda aliepata shilingi 700,000 aliimshuru Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wake huo wa kuwapa haki zao ambazo walikuwa hawatarajii kama watazipata baada ya serikali kusitisha huduma za kampuni hiyo.
Alisema Dk. Mwinyi kwa uwezo wa Allah alipewa nguvu na ilhamu kuweza kuwaangalia wananchi wanyonge ambao waliwekeza katika kampuni hiyo na kumuombea kuendelea kumpa nguvu na imani thabiti aliyokuwa nayo ili waweze kufaidika kama serikali inavyotaka.
Pili Juma Mohammed alisema uamuzi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi wa kuwarejeshea fedha zao ni jambo la busara kwani wananchi wengi wanyonge ndio waliokuwa wakiwekeza katika kampuni hiyo.
Ameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaoanzisha kampuni zisiofuta taratibu za sheria zilizowekwa nchini.
Kwa Upande wake Bwana Ame Juma Silima alisema uamuzi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwalipa wananchi wake kuwalipa fedha taslim na katika zoezi hilo na hakuna mwananchi aliekatwa.
Nae Bwana Juma Sheha Ali mkaazi wa Nungwi ambae aliweka shilingi 500,000, alisema Dk. Hussein Ali Mwinyi ni kiongozi shupavu kwani uamuzi wa kusimamia haki yao kuipata ni jambo la kupongezwa.
Alisema yeye alipatwa na wasiwasi kabla ya kwenda kuweka fedha zake katika kampuni hiyo lakini alipata ushawishi kwa baadhi ya watu ambao walikuwa wakiweka fedha katika Kampuni ya Masterlife kwa kuona ina faida ndipo alipoamua na yeye kwenda kuweka.
“Siku ya kwanza ambapo tayari nataka nipewe pesa ndipo niliposikia kwamba serikali imeifungia Kampuni nilipatwa na mshituko lakini leo nashukuru haki yangu ambayo sikutegemea kama nitaipata nimeipata ikiwa kamili,” alisema.
Mdoe Ali Haji mkaazi wa Nungwi alisema serikali kuweka utaratibu huo wa kuwarejeshea fedha zao ni jambo la busara kwa kiongozi wao na kuwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono kiongozi wao huyo kwa imani yake aliyoionesha kwa wananchi wa Zanzibar.
Hawa Ibrahim Salum alisema baada ya serikali kuifungia kampuni hiyo alipata mshituko na kuvunjika moyo lakini baada ya rais kuamua kuwalipa fedha zao na kutimiza hilo kwa vitendo.
Ziada Abdalla Hassan alimpongeza Rais Mwinyi kwa kuwaona wananchi wenye maisha ya chini waliotumbukia kwenye shimo ambalo hawakujua mwisho wake.
Alimuombea kwa MwenyeziMungu kuendelea kumpa nguvu na imani ya kuendelea kuwasaidia kwa jambo hilo na jengine na kumwambia kwamba wengi wa wananchi wameshasoma na wameshajifunza kutokana na jambo hilo lililojitokeza kwa kampuni ya masterlife.
Kwa upande wake Kamishna wa Bajeti wa Wizara Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Saumu Khatib Haji alisema katika Mkoa huo jumla ya wananchi 1,456 ambao wamepeleka fedha kiwango cha shilingi 100,000 mpaka 1,000,000 katika Kampuni ya Masterlife ambapo majira ya mchana jumla ya wananchi 310 walihudumiwa kwa kurejeshewa fedha zao.
Aliwapongeza wananchi kuendelea kuwapa mashirikiano na kuwaomba kwa siku zilizobaki katika maeneo mengine ambayo zoezi hilo litapita kuiga mfano wa mkoa huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahamoud alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kubeba dhima ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kuweza kupata haki zao ambazo zilipotea kutokana na kampuni hiyo.
Alisema Rais Mwinyi aliibeba dhima hiyo kwa kuleta utulivu katika nchi lakini kuwafanya wananchi wake waendelee na shughuli nyengine za kiuchumi na kimaendeleo kupitia fedha walizoziweka kupitia kampuni hiyo.
Mkuu Ayoub alibainisha kwamba utekelezaji wa agizo la Rais kulipwa wananchi fedha zao ni kuwasaidia wanyonge kuona wanapata haki zao bila ya usumbufu wa aina yoyote kwani kupata haki yao inasaidia kurudi katika maisha yao ya kawaida.
Hivyo aliwaomba wananchi kuwa makini katika kujiunga na kampuni zisizofuata utaratibu ili kuepusha athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
“Hili serikali limeshalibeba lakini muwe makini na watu ambao wahawana dhamira njema na mnaposikia msikurupuke kwanza mjiridhishe katika tasisi za serikali ili ukiingia uweze kubaki salama,” alisisitiza.
Mkuu Ayoub aliahidi kwamba zoezi hilo litakwenda vizuri kwa muda wa siku tatu na wananchi watapata haki yao kwa salama na amani kama ilivyopangwa na serikali.