Charles Gishuli (kushoto),Khamis Mgeja, katikati akifafanua na Mandwa Khalfan wakiteta jambo na Mgeja, nyumbani kwa katika Kijiji cha Nyanembe
Kada wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja (katikati) akisistiza jambo wakati wa mazungumzo yao na baadhi ya wazee wa mkoa huo waliomtembelea nyumbani kwake katika kijiji cha Nyanembe wilayani Kahama jana.Kushoto ni Charles Gishuli ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Khamis Mgeja, akisistiza jambo wakati wakizungumza na vyombo vya habari kuhusu upotoshaji unaofanywa na baadhi ya makada wa CCM dhidi ya serikali kushoto ni Charles Gishuli na kulia ni Mwandwa Khalfan.
Picha na Baltazar Mashaka
…………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Kahama
BAADHI ya wazee na makada wa Chama Cha Mapinfuzi (CCM) wa Mjini Kahama na mkoani Shinyanga wamepinga vikali kauli za kuikosoa serikali .
Kauli hizo za uķosoaji wa serikali zinadaiwa kutolewa hivi karibuni na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Humphrey Polepole.
Kauli hizo zilipingwa jana mjini Kahama na baadhi ya wazee hao kutoka maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga waliomtembelea Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Mkoa huo, Khamis Mgeja, nyumbani kwake katika Kijiji cha Nyanembe .
Ziara ya wazee na makada hao wa CCM ililenga kubadilishana mawazo na kujadili mustakabali wa nchi wakati ikitimiza miaka 60 ya Uhuru tangu tujitawale kutoka kwenye makucha ya wakoloni wa Uingereza.
Katika majadiliano yao wazee hao walielezea kusikitishwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na mmoja wa wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Humphrey Polepole wakidai zinaweza kuwa chanzo cha kuwagawa Watanzania.
Mmoja wa wazee hao ambaye aliyewahi kushika nafasi ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na kisha kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali hapa nchini, Charles Gishuli alisema kauli zinazotolewa na Mhe.Polepole zinapaswa kukemewa na Chama haraka.
Gishuli alisema, Polepole anachokifanya hivi sasa inaonesha wazi kama vile si mwanachama wa CCM na ana lengo la kutaka kuupotosha umma wa Watanzania uamini kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan hana uwezo wa kuongoza nchi.
“Huyu Polepole ameshika nafasi nyingi za uongozi ndani ya Serikali na Chama, aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya na Katibu wa Itikadi,Siasa na Uenezi Taifa,bahati mbaya sasa hivi amesahau kwamba ndani ya Chama kuna taratibu za kukosoana pale panapojitokeza jambo lolote lile lisilo la kawaida,” alidema Gishuli .
Aliongeza kuwa;“Ki utaratibu ndani ya Chama chetu (CCM) kuna slogani ya jinsi ya kukosoana,aelewe kwenye chama chetu hakuna mwenye mamlaka, mamlaka ni ya vikao, na hata alipokuwa msemaji wa CCM, alikuwa akizungumza baada ya kutoka ndani ya vikao, si kama anavyofanya hivi sasa.”
Alisema hata kama kuna makosa yamejitokeza ndani ya serikali alipaswa kutumia utaratibu uliopo ndani ya CCM na kutoa mfano wa hivi karibuni alipomkosoa Mbunge mwenzake, Nape Nnauye nje ya utaratibu.
Kwa upande wake Mgeja alisema kitendo kinachofanywa sasa na Mheshimiwa Polepole kimeonesha wazi madhara ya kuteua watu ambao hawajapata mafunzo yoyote ya kiuongozi.
Alisema yeye binafsi anashindwa kupata uhalisia wa Polepole, kutokana na kujionesha yeye ndiye mwana CCM halisi, na hata kudiriki kuwaita baadhi ya Watanzania kwamba ni wahuni na mbaya zaidi amekuwa akizungumzia kuhusu nchi baada ya Hayati John Magufuli kushindwa kuwamaliza wahuni ndani ya CCM na ndani ya nchi.
“Sasa jambo kama hili siyo la kufumbia macho, jambo hili ni uchochezi, ni upotoshaji lakini pia ni kupandikiza chuki, ukiangalia mwenendo wa Polepole anayoyazungumza hivi sasa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ni kama anataka kuupotosha umma na kuuaminisha kuwa Rais Samia hana uwezo wa kuongoza nchi,”
“Inaonesha ana lengo la kutaka kugonganisha Serikali ya Awamunya Dita iliyopo hivi sasa madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ionekane kwamba kuna tofauti kubwa kati ya serikali iliyopita na serikali iliyopo sasa, haya mambo yasipokemewa huyu mtu tutampa nafasi kubwa ya kulipotosha Taifa,” alieleza Mgeja.
Aliendelea kueleza kuwa Mheshimiwa Polepole ana lengo la kutaka aonekane yeye ndiye mwanachama safi wa CCM na msema kweli ambapo kiuhalisia ndani ya Chama cha Mapinduzi hana historia yoyote kwa vile kabla ya kuteuliwa katika nafasi ya uongozi wa juu ndani ya CCM hakuwahi kuwa hata Katibu Tawi wa CCM.
Mgeja alisema ni vyema Polepole akajirudi ambapo alikiomba Chama cha Mapinduzi kiangalie uwezekano wa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa vile kauli anazozitoa zinaweza kuharibu mustakabali wa Taifa la Tanzania pasipo sababu za msingi.
Katika hatua nyingine wazee hao wameelezea kushangazwa na kauli zinazototolewa na baadhi ya Watanzania wakimlaumu Rais aliyepo madarakani kwamba amekuwa akisafiri mara kwa mara tofauti na mtangulizi wake Hayati John Magufuli.
“Ni mambo ya ajabu kudai Rais anasafiri sana, wanaotoa madai haya hawaelewi umuhimu wa mahusiano ya Kimataifa, ili nchi iwe na maendeleo ya haraka lazima iwe na mahusiano na mataifa mengine makubwa ikiwemo suala la kutafuta wawekezaji,” alieleza Charles Gishuli.
Aifha Mgeja yeye alisema wanaolalamikia safari za Rais Samia ni wavivu wa kufikiri, kwa vile nchi ya Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa na kwamba Taifa la Tanzania bado halijasimama vizuri kiuchumi.
“Tanzania bado hatujasimama kiuchumi, tunatakiwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi za nje, Rais Samia hivi sasa kazi hiyo anaifanya vizuri, ndiyo maana sasa watu wengi wanavutika kuja kuwekeza hapa nchini, na hata suala la kukopa, ukitaka kuendelea lazima ukope,” alieleza Mgeja.
Kuhusu miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania wazee hao walisema Taifa linakwenda vizuri na limepiga hatua katika sekta za afya, elimu, miundombinu ya barabara na hali ya amani na utulivu imeendelea kuimarika kutokana na uongozi bora uliopo .
Kwamba kutokana na hali hiyo watu wachache wapotoshaji na wapinga maendeleo hawapaswi kupewa nafasi ya kuishanbulia serikali bila sababu za msingi.
Naye mzee Said Hamad mkazi wa Mondo, Kahama Shinyanga yeye alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna ilivyojikita katika suala la kuboresha elimu na huduma za afya kwa kujenga shule, zahanati na vituo vya afya bila kuwachangisha wananchi.
“Kuelekea miaka 60 ya uhuru mimi nimefurahishwa na kuridhishwa sana na utendaji wa Serikali hii ya awamu ya sita, ndani ya kipindi kifupi imefanya mambo makubwa upande wa hufuma za jamii (elimu na afya), vyumba vya madarasa vimejengwa zaidi ya 14,000 ndani ya mwezi mmoja,” alisema .