*****************************
Na Victor Masangu,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema kwamba katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru kuna mafanikio mbali mbali ambayo yameweza kujitokeza katika sekta mbali mbali ikiwemo afya,elimu,miundombinu ya maji pamoja na ujenzi wa viwanda vipatavyo 1438.
Kunenge ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru kimkoa ambayo yamefanyika katika viwanja vya mail moja Wilayani Kibaha na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali wakiwemo wakurugenzi na viongozi wa dini sambamba na wananchi.
Aidha Kunenge alisema kuwa katika kipindi chote cha miaka 60 Mkoa wa Pwani umeweza kuwa kinara wa kuongoza kwa uwekezaji wa viwanda mbali mbali ambavyo vimejengwa na vinadaidia kwa kiasi kikubwa kukuza pato la Taifa.
Kunenge alifafanua kwamba lengo kubwa la serikali ya Mkoa wa Pwani ni kuhakikisha kupitia maadhimisho haya itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani ya nchi pamoja na wale wa nje ili kutengeneza fursa za ajira.
Kadhalika aliongeza kuwa licha ya kuongoza katika sekta ya viwanda pia wameweza kufanya vizuri katika sekta ya kilimo na ufugaji ambapo kwa Sasa Kuna mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki yapo120.
Alifafanua kuhusiana na suala la upatikanaji wa maji Safi na salama alisema kuwa umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo kwa Sasa katika maeneo ya Mkoa wa Pwani maji yanapatikana kwa kiwango cha asilimia zipatazo 84.
Kuhusiana na sekta ya elimu Kunenge hakusita kuweka wazi mafanikio ambayo yameweza kuonekana ambapo shule mbali mbali za msingi zimejengwa ikiwemo sambamba na ujenzi wamiradi ya nyumba za walimu lengo ikiwa ni kuboresha sekta ya elimu.
Katika hatua nyingine amesema kwamba atalivalia njuga suala la baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuwa matapeli wa ardhi na kwamba atahakikisha anawachukulia hatua Kali kwa mujibu wa sheria na taratibu bila kumwonea .mtu yoyote Yule.
Sambamba na hilo alisema kuwa katika kipindi Cha miaka 60 ya Uhuru Mkoa wa Pwani hadi Sasa umefanikiwa kujenga zahanati zipatazo 262 pamoja na vituo vya afya 44.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Msafiri alifafanua kuwa kwa kipindi chote cha miaka 60 Kuna Mambo mengi ambayo yamefanyika katika miradi ya maji,afya,umeme,miundombinu ya barabara na uboreshaji wa huduma za kijamii.