******************************
Na Sixmund J. Begashe
Naibu Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini zamani Swaziland, alieambatana na Mkewe Bi Dimpho Masuku na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Thulisile Dlodla wameitembelea Makumbusho ya Taifa ili kujionea uhifadhi adhimu wa historia ya nchi na urithi wa asili na utamaduni uliohifadhiwa na kuoneshwa Makumbusho na Nyumba ya Utamadani Dar es Salaam.
Mhe Masuku alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw Achiles Bufure kisha kutembezwa kwenye kumbi mbalimbali zilizo beba Historia ya nchi, Chimbuko la Mwanadamu, Sanaa, michoro ya mapangoni, Bustani ya Vipepeo, na Maktaba ya kihistoria.
Akiwa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Mhe. Masuku na mkewe walipata nafasi pia ya kuingia chumba mahususi ambako walijionea fuvu la binadamu wa kale Zinjanthropus anaesadikiwa kuishi miaka milioni 1.7 iliyo pita, hati ya Uhuru, tai zilizovaliwa siku ya Uhuru, vifaa vilivyotumika kuchanganyia udongo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar nk.
Baada ya ziara hiyo Mhe Masuku aliipongeza Makumbusho ya Taifa kwa hatua kubwa iliyo piga katika uhifadhi wa urithi wa Utamaduni na wa Malikale, huku akimwagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe Thulisile Dlodla kuhakikisha ofisi yake inaipatia Makumbusho ya Taifa taarifa na nyaraka muhimu zinazo husu usafirishwaji wa watumwa kwenye Miji ya Lusaka, Nairobi na Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga amemshukuru Mhe Masuku na Ujumbe wake kwa kuona umuhimu wa kuitembelea Makumbusho ya Taifa ili kujifunza na kujionea uhifadhi wa urithi adimu na adhimu unao husu utamaduni na malikale za Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla. Sanjari na pongezi hizo, Dkt Lwoga alimpatia Mhe Masuku zawadi ya vitabu vya historia pamoja na Vikombe vyenye kauli mbiu za program zinazoendeshwa na Taasisi yake.
Naibu Waziri Mkuu huyo Mhe Masuku yupo hapa nchini kumwakilisha Mfalme Mswati wa Tatu katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania yanayo tarajiwa kuadhimishwa kitaifa Desemba 9 Mkoani Dar es Salaam ambapo Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani atakuwa mgeni Rasmi.